• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Kenya yachukua ubingwa katika soko la mihadarati

Kenya yachukua ubingwa katika soko la mihadarati

Na AFP

KENYA imegeuka kuwa soko kubwa na kitovu cha matumizi ya mihadarati, baada ya walanguzi kuhofia ulinzi mkali uliopo katika mipaka ya bara Uropa ambayo walitegemea zamani.

Mkazi wa Nairobi, Bi Esther Wanjiru anasimulia kuwa alianza kutumia dawa za kulevya aina ya heroini akiwa na umri wa miaka 16 ili kupunguza mawazo baada ya mwanawe kufariki.

Alianza kuivuta kama sigara kabla ya kuanza kujidunga dawa hiyo ambayo imeanza kupatikana kwa wingi na kwa gharama ya chini nchini Kenya.

“Mimi ni mraibu wa dawa hii, huhitaji dozi mbili kila siku,” akasema Wanjiru, 22, anapojidunga dawa hiyo huku akizingirwa na wenzake 60 nyuma ya kanisa moja katika mtaa mmoja wa mabanda, Nairobi.

Japo zamani Kenya ilikuwa ikitumiwa na walanguzi kupitisha heroini hadi Uropa, nchi hii imegeuka kuwa soko la dawa hiyo ya kulevya, idadi wa waraibu ikiongezeka huku tani kadhaa zikifikishwa nchini humu.

Siku hizi kipimo kimoja kinagharimu Sh120 pekee, hali inayochangia Wakenya maskini kama Wanjiru kuipata kwa urahisi. Wanjiru anasema hufanya kila awezalo ili kupata pesa za kununua dawa hiyo, ikiwemo kujiingiza katika uhalifu na ukahaba.

Heroini ilikuwa ikifika Uropa kupitia ukanda wa Balkan, kutoka Afghanistan kupitia Mashariki ya Kati hadi miji mbalimbali ya mataifa ya bara hilo.

Lakini mapigano nchini Syria na ulinzi mkali kwenye mipaka kufuatia wimbi la wahamiaji kutafuta hifadhi Uropa uliwalazimu walanguzi kubadili mbinu za kuingiza dawa hiyo barani humo.

Walanguzi walilazimika kutumia usafiri wa bahari ili kukwepa kuzuiwa katika maeneo ya mipaka.

Heroini ilisafirishwa kwa meli kupitia Bahari Hindi hadi pwani ya Afrika Mashariki, kisha ikasafirishwa hadi Uropa. Mombasa ilikuwa njia kuu ya kusafirisha dawa hizo.

Japo Kenya ni nchi ya usalama wa hali ya juu, kukithiri kwa ufisadi na utepetevu wa maafisa wa usalama uliwawezesha walanguzi kuingiza bidhaa hiyo.

“Walanguzi wa dawa za kulevya wametambua Kenya kama mojawapo ya nchi salama katika ukanda huu kwa biashara yao,” akasema Amado De Andres, aliyekuwa mkurugenzi wa kanda ya Afrika Mashariki katika Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Dawa na Uhalifu (UNODC).

Shirika hilo linakadiria kuwa tani 42 za heroini ambazo hufikishwa Kenya kila mwaka zilikuwa zikinuiwa kuuzwa katika masoko ya mbali.

Lakini baada ya muda, hitaji la dawa hizo hapa nchini lilianza kupanda. Walanguzi walitenga karibu tani tano za heroini kwa ajili ya kuuzwa humu nchini huku soko lake likiendelea kupanuka na kufikia biashara ya thamani ya Dola 150 milioni (Sh15 bilioni).

“Awali, Kenya ilikuwa njia ya kupitishia tu, lakini sasa imegeuka kuwa soko kubwa la heroini,” akasema Victor Okioma, Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Pombe na Mihadarati (NACADA).

Mnamo 2018, Wizara ya Afya ilikadiria kuwa jumla ya watu 27,000 walikuwa wakijidunga ua kuvuta heroini. Uchunguzi huo ulifanyika katika karibu kaunti 15 kati ya kaunti zote 47.

Lakini shirika lisilo la kiserikali la kupambana na Uhalifu Ulimwengu, Global Initiative Against Transnational Organized Crime lilikadiria kuwa jumla ya watu 55,000 walikuwa wakijidunga dawa hiyo, ishara kwamba idadi ya watumiaji dawa hiyo ilikuwa juu.

Kwa sasa heroini ni dawa ya pili ya kulevya inayotumiwa na watu wengi zaidi Kenya; bangi ikiongozwa kwa kutumiwa na zaidi ya watu 50 milioni.

  • Tags

You can share this post!

Machifu sasa kulipwa pesa za kuinua motisha

NASAHA ZA RAMADHAN: Si lazima watu kukesha msikitini wakati...