• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Serikali yasisitiza kufungua shule Jumatatu

Serikali yasisitiza kufungua shule Jumatatu

Na WANDERI KAMAU

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha, amesititiza kuwa shule zote zitafunguliwa Jumatatu kama ilivyopangwa, wala hakutakuwa na mabadiliko yoyote.

Kumekuwa na uvumi kwamba huenda serikali ikabadilisha tarehe hiyo kutokana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini.

Lakini kwenye kikao na wanahabari katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Starehe, Nairobi, Ijumaa, Prof Magoha alisema kuwa ratiba ya masomo itaendelea kama ilivyopangwa ili kuwawezesha wanafunzi kutopoteza muda wowote kama mwaka uliopita.

Kauli yake inawiana na agizo lililotolewa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumamosi iliyopita kwamba tarehe hiyo haitabadilishwa.

“Tunataka kuhakikisha ratiba ya masomo nchini imerejea kama ilivyokuwa awali. Vile vile, tunataka kuhakikisha mitihani ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) imefanywa mwaka huu 2021. Tukiwa katika mwezi Mei, muda umesonga sana. Hivyo, hatutafanya lolote ambalo litavuruga na kupangua ratiba yetu,” akasema.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Wizara ya Elimu, muhula wa tatu utaisha Julai 16.

Wanafunzi watakaorejelea masomo Jumatatu ni wale wa PP1 na PP2, Darasa la Kwanza hadi Tatu, Darasa la Tano hadi Saba na Kidato cha Kwanza hadi cha Tatu.

Wanafunzi wa Darasa la Nne wataendelea kukaa nyumbani hadi Julai 26, wakati shule zitakapofunguliwa upya kwa muhula wa kwanza 2021.

Baada ya kufungua, wanafunzi wataendelea na masomo yao hadi pale watakapoenda likizo nyingine fupi kati ya Oktoba 2 hadi Oktoba 10.

Watarejea shuleni kwa muhula wa pili ambao utaendelea hadi Desemba 23.

Ratiba ya kawaida inatarajiwa kurejelewa Januari 2023.

Hilo linamaanisha kutakuwa na mihula minne ya masomo katika mwaka wa 2022, badala ya mihula mitatu kama ilivyo kawaida.

Mwaka uliopita, wanafunzi walikaa nyumbani kwa karibu miezi kumi kutokana na tishio za virusi hivyo hatari. Kando na hayo, waziri aliwaagiza walimu wakuu katika shule zote kuhakikisha wameweka mikakati ifaayo ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona miongoni mwa wanafunzi.

Ili kufanikisha hilo, alisema serikali imetoa Sh7.5 bilioni ambazo watapata kufikia wiki ijayo.

Alisema wametuma maombi kwa Hazina ya Kitaifa kuwapa Sh13 bilioni na Sh2.8 bilioni kwa shule za upili na msingi mtawalia zitakazotumika katika muhula wa tatu.

“Sitaki kusikia visingizio vyovyote kwamba kuna shule ambayo haijaweka tahadhari na matayarisho yafaayo kwa ukosefu wa fedha. Tushatuma fedha hizo kwa akaunti za shule zote na tunatarajia mtazipata mapema wiki ijayo,” akasema.

Waziri pia alitangaza shughuli ya kuwapa chanjo walimu itaendelea kama ilivyopangwa, baada ya Kenya kupokea shehena ya pili ya chanjo hizo.

Kufikia sasa, karibu nusu ya walimu kote nchini wamepewa chanjo, ikizingatiwa wameorodheshwa kuwa miongoni mwa makundi muhimu yanayopaswa kuchanjwa kwanza.

Wakati huo huo, alisema usahihishaji wa mtihani wa KCSE mwaka huu 2021 umekamilika, na wizara itaeleza kuhusu ni lini itatangaza rasmi matokeo hayo.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti kupokonywa chanjo zipelekwe kwingine

MAKALA MAALUM: Corona ilipogonga riziki za wengi, ubunifu...