Polo atorokwa na demu juu ya msoto

Na TOBBIE WEKESA

ROASTERS, Nairobi

POLO mmoja alilazimika kula kwa macho baada ya kidosho aliyekuwa akiburudika naye katika baa kuhamia meza ya makalameni wengine iliyojaa pombe.

Kidosho alichukua hatua hiyo baada ya kugundua kwamba jamaa alikuwa ameishiwa na hela za kununua chupa zaidi za pombe.

Kulingana na mdokezi jamaa na mrembo waliingia katika baa na kuitisha vinywaji. Waliagiza nyama choma vile vile.

Duru zinasema baada ya kubugia chupa kadhaa, kidosho alimhimiza polo aongeze vinywaji vingine.

Beib mimi sipendi kuona meza ikiwa wazi hivi. Hebu jaza meza iwe jinsi ilivyokuwa hapo awali,” kidosho alimueleza jamaa.

Lofa alijitia hamnazo. Baada ya muda mfupi kidosho alimkumbusha. “Beib hebu muite weita. Hii meza inatupa aibu. Ongeza pombe,” kidosho alimueleza polo.

Duru zinasema jamaa alimuangalia kidosho na kunyamaza.

“Kama pesa zako zimeisha niambie. Ni wewe uliniita kulewa na unajua mimi hunywa chupa ngapi. Siko tayari kurudi kwa nyumba saa hii,” kidosho alimfokea polo.

Habari zilizotufikia zinasema kidosho aliinuka polepole na kuelekea hadi kwenye meza walikokuwa wameketi makalameni fulani.

“Karibu sana mrembo. Meza hii imeketi wanaume kamili,” kalameni mmoja alisikika akimuambia kidosho.

Kidosho aliwashukuru kwa ukarimu wao.

“Asanteni sana. Yule jamaa ni mtu wangu lakini anakaa mkono birika sana. Siwezi kaa kwenye meza yenye haina raha,” kidosho alisema huku vicheko vikishamiri.

Inadaiwa makalameni waliitisha vinywaji zaidi.

“Weita jaza hii meza na ulete bili. Leo lazima watu watembee kwa magoti,” kalameni mmoja alisema.

Polo alibaki kutazama jinsi makalameni walivyomuosha kidosho wake kwa pombe. Muziki uliwekwa. Kidosho aliinuka na kuanza kuwaburudisha makalameni kwa miondoko mbalimbali ya kusakata densi.