• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Waandishi wanaofanyia kazi zao Kiambu wapewa hamasisho

Waandishi wanaofanyia kazi zao Kiambu wapewa hamasisho

Na LAWRENCE ONGARO

WAANDISHI wa habari wanaofanya kazi wakiwa eneo la Kiambu, wamehimizwa kuwa mstari wa mbele kuandika na kuripoti habari zilizo sahihi na za ukweli kwa lengo la kusambaza habari kwa umma.

Mkuu wa Ustawishaji Vyombo vya Habari na Mikakati katika Baraza la Vyombo vya Habari (MCK), Bw Victor Bwire, alisema mwandishi kamili wa habari anastahili kupata habari kamili kutoka kwa mhusika wala sio kuangazia mambo ya kusikia kutoka kwa watu.

“Wewe kama mwandishi wa habari unastahili kufika eneo la tukio na kukusanya habari kamili kuhusu yale yanayotendeka ili baadaye uandike habari kamili na sahihi. Usikubali kuchukua habari zisizo na ukweli,” alisema Bw Bwire.

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa katika hoteli moja mjini Ruiru alipofanya mkutano na waandishi wa habari wapatao 30 wanaofanya kazi mara nyingi wakiwa Kaunti ya Kiambu.

Alitoa changamoto kwa waandishi wa habari katika eneo hilo kuwa makini sana wanapoangazia habari muhimu za chaguzi ndogo za Juja na Kiambaa, ambazo zinatarajiwa kuendeshwa hivi karibuni.

Alitoa mfano wa uchaguzi wa eneobunge la Kiambaa unaotarajiwa baada ya kifo cha Mbunge Paul Konange.

Alisema kwa sasa kiti hicho kinagombaniwa na wawaniaji 11 ambapo watatu kati yao wanatoka katika familia moja ya Koinange.

“Iwapo unaripoti maswala kuhusu wawaniaji wa kiti hicho ni lazima ufanye juhudi kuona ya kwamba kila mmoja anapata nafasi ya kuangaziwa kwa usawa ili kuonyesha uwazi kwa kila mmoja,” alisema Bw Bwire.

Waandishi pia walishauriwa wawe makini sana wakati wa kuuliza maswali kwa sababu “ukikosa kuelewa jinsi ulivyoelezwa utatoa habari zisizo sahihi.”

Alisema pia kuna haja ya kujaribu kufuatilia maswala ya maendeleo mashinani badala ya kuzamia sana kwa mambo ya siasa.

“Wananchi mashinani wanahitaji maji, stima, barabara nzuri na kadhalika na hayo ndiyo wangetaka kuelezewa zaidi kuliko maswala ya siasa. Hata wakati mwingi unapomhoji kiongozi yeyote jaribu kuchangamkia maswala ya maendeleo,” alisema afisa huyo wa MCK.

Waandishi pia walishauriwa kuweka usalama wao na afya mbele hasa wakati huu wa homa kali ya Covid-19, kwani wao pia wanaweza kupatikana na shida wakati wowote.

Afisa anayechambua habari zisizo sahihi Bw Leo Mutisya, aliwahimiza waandishi wawe makini wasije wakanaswa na mtego wa kuandika habari chwara zinazoweza kuleta shida kwa mwandishi mwenyewe na mwajiri wake vile vile.

“Kuna vituo vya habari vingi ambavyo vimefungwa na hata kutozwa faini za juu baada ya waandishi wao kuangazia maswala yasiyoambatana na habari kamili,” alisema Bw Mutisya.

Mwanahabari pia amehimizwa kufanya kazi na wenzake badala ya kwenda kwenye tukio akiwa peke yake.

Alisema habari chwara siku hizi zimeteka nyara mitandao ya kijamii na kwa hivyo ni vyema mwandishi wa habari kuwa makini pia anapozisoma.

You can share this post!

Zesco yazoa ushindi wa10 mfululizo ligini Zambia, Were,...

Majonzi 18 wakifa ajalini