• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Watahiniwa watumia mbinu mpya za wizi KCSE

Watahiniwa watumia mbinu mpya za wizi KCSE

Na WANDERI KAMAU

BARAZA la Kitaifa la Mitihani (KNEC) limefutilia mbali matokeo ya wanafunzi 287 kwenye Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka uliopita, baada yao kupatikana wakitumia mbinu mbalimbali za kushiriki kwenye udanganyifu.

Hata hivyo, idadi hiyo ilipungua pakubwa ikilinganishwa na 2019, ambapo jumla ya visa 1,039 viligunduliwa.Kulingana na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, baadhi ya visa vilihusisha walimu kutumia simu zao kupiga picha mitihani na baadaye kutuma maswali kwa wanafunzi.

Baadhi ya mbinu zilizotumika kuendeleza udanganyifu huo ni matumizi ya vifaa visivyoruhusiwa kwenye vyumba vya mitihani, matumizi ya simu, watu kuwafanyia wale wengine kati ya zingine.

Profesa Magoha alisema walinasa jumla ya simu 45 za rununu ambazo zilitumika kushiriki udanyanyifu, ikilinganishwa na 47 mnamo 2019.Watu 211 ndio walipatikana wakitumia vifaa ambavyo haviruhusiwi kwenye vyumba vya mitihani.

Ili kukabili maovu hayo, waziri alisema wanalenga kuanzisha mfumo mpya wa kiteknolojia, ambapo yeyote atakayefungua karatasi za mtihani kabla ya muda uliopangwa atanaswa mara moja kupitia alama zake za vidole.

“Tunashirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) kuweka mfumo wa kiteknolojia ambapo itakuwa rahisi sana kuwanasa wale wanaofungua karatasi za mitihani bila idhini,” akasema.

You can share this post!

Viongozi Pwani watafutia Ruto mgombea mwenza

Wasichana wazidi idadi ya wavulana katika KCSE Kwale