• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Ruto alenga waasi wa Odinga Luo Nyanza

Ruto alenga waasi wa Odinga Luo Nyanza

Na CECIL ODONGO

NAIBU Rais Dkt William Ruto amerusha chambo chake katika ngome ya Kinara wa ODM Raila Odinga ya Luo Nyanza, baada ya wandani wake kutoka jamii ya Waluo kuandaa mkutano na viongozi wa zamani ili kutoa mwelekeo wa kufufua uchumi wa eneo hilo.

Mfanyabiashara Eliud Owalo na mbunge wa zamani wa Rangwe Martin Ogindo waliongoza mkutano huo uliofanyika katika hoteli moja jijini Nairobi.

Aliyekuwa Gavana wa Kisumu Jack Ranguma, waziri wa zamani Dalmas Otieno pamoja na wasomi na wataalamu kutoka eneo hilo walishiriki mkutano huo.

Hata hivyo, kilichodhihirisha kuwa mikakati ya kisiasa ya 2022 inapangwa ni kauli ya Bw Owalo kwamba, mwaniaji yeyote anayesaka Urais na uungwaji mkono wa Waluo, atalazimika kutia saini mkataba wa kusaidia eneo hilo kuimarika kiuchumi iwapo atafanikiwa kuingia afisini.

Pia, walisisitiza kwamba viongozi wanaowania kiti cha ugavana lazima wawe wasomi ambao wanaelewa masuala ya uongozi. Wasomi na wanasiasa walioshiriki mkutano huo wanatoka katika kaunti za Kisumu, Siaya, Homa Bay na Migori.

“Mtu yeyote anayegombea Urais atalazimika kuzungumza nasi ili kabla ya kumuunga mkono kwa kiti cha Urais, atatia saini mkataba wa kutimiza ahadi zote alizotoa kwetu akiingia afisini,” akasema Bw Owalo.

Hata hivyo, kauli hiyo huenda ikawagonganisha na wanasiasa wa ODM na viongozi kwenye mrengo wa Bw Owalo ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakimpiga vita Bw Odinga.

Pia itakuwa vigumu kwa Bw Odinga kuridhia ombi la mrengo huo la kutia saini mkataba huo kwa kuwa ana uungwaji mkono mkubwa katika eneo hilo wala si rahisi kwa mwanasiasa yeyote kuamua kinyume cha agizo lake.

Hata hivyo, mkutano huo unafasiriwa kama njia ya kuwashawishi wakazi wakubali wawaniaji wengine wa Urais akiwemo Dkt Ruto kunadi sera zao eneo hilo bila upinzani wowote.

Mabw Otieno, Ogindo na Owalo ni waasi wa ODM na hatua ya Bw Ranguma ambaye duru zinaarifu analenga kiti cha useneta wa Kisumu, huenda ikamsawiri kama aliyejiunga na mrengo wa Tangatanga.

Kufufua viwanda vya sukari, kilimo cha pamba na mpunga, kuinua kwa viwango vya elimu, utalii na miundomsingi ni kati ya miradi Bw Owalo alisema kundi lake linalenga kuangazia.

You can share this post!

Mradi wa Uhuru 2022

Wazazi watozwa ng’ombe 100 kwa utundu wa watoto wao