• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
TAHARIRI: Serikali iwasaidie waliokwama India

TAHARIRI: Serikali iwasaidie waliokwama India

KITENGO CHA UHARIRI

SERIKALI inapaswa kusikia vilio vya Wakenya waliokwama nchini India na kuwasaidia kurejea nchini ili kuwawezesha kuendelea na maisha yao.

Mamia ya Wakenya wamekuwa wakilalamika kuhusu ugumu wa maisha wanaopitia nchini humo, tangu serikali iliposimamisha safari za ndege kuelekea huko mapema mwezi huu; Mei.

Wengi kati yao walikuwa wamesafiri India kutafuta huduma za matibabu kwa magonjwa kama saratani, kutokana na kiwango bora cha huduma za afya nchini humo.

Serikali ilisimamisha safari hizo kutokana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona katika taifa hilo, ikilenga kuwalinda Wakenya dhidi kuambukizwa.

Ikizingatiwa kuwa aina ya corona iliyogunduliwa India imetajwa kuwa hatari kuliko virusi vilivyopatikana katika sehemu nyingine duniani, serikali ina haki ya kuhakikisha raia wake wako salama.

Hata hivyo, ni muhimu taasisi husika, hasa Wizara ya Mashauri ya Kigeni, kufahamu kuwa Wakenya wote hawakufanikiwa kurejea nchini katika muda ambao serikali ilitoa.

Baadhi yao walikuwa wamepangiwa kufanyiwa upasuaji na matibabu maalum kutokana na aina ya maradhi yao, hivyo lazima wangeendelea na matibabu hayo.

Kutokana na hali ngumu zinzowakabili wale waliokwama huko, wengi wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuelezea masaibu wanayopitia. Miongoni mwa changamoto hizo ni ukosefu wa fedha, kwani kila kitu katika nchi ya kigeni huwa ni gharama.

Vibaya zaidi, ni wakati mtu anapokuwa hana ajira maalum ama fedha alizokuwa nazo zimeisha na hana namna ya kurejea kwao kutokana na vikwazo vilivyowekwa.

Katika mazingira magumu kama hayo, Wakenya hao hawana namna ila kuililia serikali, jamaa na marafiki wao kuwasaidia kwa namna yoyote ile wanayoweza.

Ikizingatiwa kuwa tumeona serikali ikituma ndege kuwasaidia Wakenya waliokwama katika nchi kama Sudan Kusini, tunatoa wito kwa idara husika kuwasaidia walio India kurejea nchini.

Kwa kuwa wengi wanakumbwa na changamoto za kifedha, tunairai pia kuwasaidia kulipia gharama muhimu kama vile ada za karantini, kwani watalazimika kutengwa kwa muda ili kuhakikisha hawaajambukizwa virusi hivyo.

Hivyo ndivyo, itaonyesha kuwa inawalinda, kuwathamini na kuwajali raia wake, bila kujali asili wala hadhi yao katika jamii.

You can share this post!

Uvundo tele Nairobi huku NMS ikizembea

Vipusa wa Barcelona wakomoa Chelsea 4-0 na kutwaa taji la...