Demu aachwa kwa kukwamilia mzinga

Na TOBBIE WEKESA

MWIKI, NAIROBI

KIDOSHO mmoja hakuamini mpenzi wake alipomuacha mataani kwa kukataa kumtimizia haja zake.

Inasemekana polo aliamua kumuacha baada ya kugundua kwamba kidosho alikuwa akimfyonza mali ilhali hakuwa tayari kumfungulia mzinga arambe asali.

Kulingana na mdokezi, polo na kidosho walikutana katika hoteli ilivyokuwa kawaida yao.

“Mimi ningependa kunywa juisi. Wewe itisha chakula chako,” polo alimueleza kidosho.

Kidosho aliitisha menu na kuanza kuikagua kwa makini. Weita aliwakaribia.

“Mimi niletee juisi baridi na samosa moja,” polo alimueleza weita.

Inadaiwa baada ya kupitisha jicho lake kwenye kurasa zote za menu, kidosho aliagiza chakula.

“Naomba uniletee wali kwa samaki,” kidosho alimueleza weita.

Baada ya muda mfupi mlo uliletwa.

“Beib leo utalala kwangu. Acha niitishe teksi,” polo alimueleza kidosho huku wakiendelea kula.

Duru zinasema totoshoo aliinuka na kumtazama polo.

“Beib najua unachotaka. Hakuna haraka kwa hayo mambo. Kuwa mpole,” alimweleza jamaa.

Inadaiwa jibu la kidosho halikumfurahisha polo.

“Beib tangu tuanze kupendana karibu tunamaliza mwaka mmoja. Kila wakati ukija kwangu unaniambia nisubiri. Nitasubiri hadi lini?” polo alifoka.

Kidosho alijitia hamnazo.

“Juzi ulikuja kwangu. Nikagharamika sana lakini hata busu pekeyake hukunipa,” polo alimfokea kidosho.

Kidosho aliendelea kushambulia chakula. Hakujali maneno ya polo.

“Huwezi kuendelea kuninyonya huku vya kwako ukivifungia kwa kufuli. Tafuta mchumba mwingine,” polo alifoka.

Polo hakumpa kidosho muda kujitetea.

“Kila wakati unasema “nitakupa siku moja”. Kwani hiyo siku ni lini? Nimevumilia ya kutosha. Usiwahi kunipigia simu,” polo alimwambia kidosho huku akiamka na kuenda zake.