• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Malalamiko ya ODM uchaguzi mdogo Bonchari

Malalamiko ya ODM uchaguzi mdogo Bonchari

WYCLIFFE NYABERI na SAMMY WAWERU

SHUGHULI ya uchaguzi mdogo katika eneobunge la Bonchari, Kaunti ya Kisii imeanza Jumanne asubuhi.

Vituo vya kupigia kura vipatao 103 vilifunguliwa saa kumi na moja alfajiri lakini shughuli yenyewe ikaanza saa kumi na mbili asubuhi.

Hali ya usalama imeimarishwa vilivyo kutokana na ripoti zilizochipuka kwamba baadhi ya wahuni walikuwa wakipanga kuzua fujo kwenye uchaguzi huo.

Polisi wameweka vizuizi vingi kwenye barabara zinazoingia Bonchari.

Kuliibuliwa madai ya uhongaji wa wapiga kura katika kituo kimoja cha Nyamiobo, kinachopatikana Wadi ya Riana.

Ajenti wa ODM alidai kwamba baadhi ya mawakala wa mwaniaji fulani alikuwa akipeana pesa kwa wapigakura waliokuwa kwenye foleni.

Naye Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amesema yuko mafichoni, akidai kusakwa na polisi ili kutiwa nguvuni.

Kwenye mahojiano na runinga ya KTN News, Sifuna amelalamikia ODM kuhangaishwa na serikali kwa kile ametaja kama “njama ya Jubilee kutwaa kiti cha ubunge Bonchari kwa kutumia nguvu za kimabavu”.

“Chama cha ODM kipo tayari kukubali matokeo ya huru na haki, ila hatutakubali kunyanyaswa na maajenti wetu kukamatwa bila sababu na maafisa wa polisi,” Sifuna akasema, akidokeza yuko mafichoni.

“Jubilee inataka kuchukua kiti kwa nguvu, uchaguzi huu si wa huru na haki,” akateta.

Katibu huyo ameibua madai ya udanganyifu na wapiga kura kuhongwa, tetesi ambazo amehoji zinasakatwa na maafisa wa serikali.

Sifuna amepinga madai kuwa anasakwa na polisi baada ya kupatikana na pesa ikidaiwa alinuia kuhonga wapigakura.

Kamanda wa polisi wa eneo la Nyanza Bw John Muiruri amekiri kutiwa mbaroni kwa watu kadhaa waliopatikana wakiwahonga wapigakura usiku wa kuamkia Jumanne.

“Tumewanasa watu kadhaa na pesa walizokuwa nazo. Hawatasazwa na watafikishwa mahakamani. Jukumu letu ni kuweka amani, ” akasema Bw Muiruri.

Mwaniaji wa chama cha Jubilee Bw Zebedeo Opore, ambaye amekuwa akilaumiwa na wagombea wenza kwamba serikali imekuwa ikimlinda na kumpigia debe, aliyakana madai kuwa yeye ni mradi wa serikali katika uchaguzi huo.

“Ni nani asiye mradi wa chama chake? Mimi ni mwanachama wa Jubilee na chama changu lazima kinivumishe jinsi vifanyavyo vyama vingine, ” akasema Bw Opore.

Eneobunge la Bonchari lina wapiga kura 52,095 waliogawanyika kwenye wadi nne ambazo ni Bomorenda, Bogiakumu, Riana na Bomariba.

Zebedeo Opore ndiye anapeperusha bendera ya Jubilee, Pavel Oimeke (ODM)) na Teresa Oroo Bitutu (UDA).

Wagombea wengine ni pamoja na Mary Otara (UGP), Jonah Ondieki (New Democrats), Victor Omanwao (PED), Charles Mogaka (PPK), David Ogega (KSC), Kevin Mosomi wa PDU, na Eric Oigo (National Reconstruction Alliance).

Kiti cha ubunge Bonchari kilisalia wazi baada ya kifo cha mbunge John Oroo Oyioka, mnamo Februari 15, 2021.

You can share this post!

Jeraha la goti kumnyima kigogo Zlatan Ibrahimovic uhondo wa...

Cavani sasa kuchezea Manchester United hadi Juni 2022