• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Jeraha la goti kumnyima kigogo Zlatan Ibrahimovic uhondo wa kipute cha Euro

Jeraha la goti kumnyima kigogo Zlatan Ibrahimovic uhondo wa kipute cha Euro

Na MASHIRIKA

NYOTA Zlatan Ibrahimovic hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachowakilisha Uswidi kwenye fainali za Euro mwaka huu 2021 kwa sababu ya jeraha la goti.

Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 39 alirejea katika kikosi cha uswidi mnamo Machi 2021 baada ya kubatilisha maamuzi yake ya awali ya kustaafu kwenye soka ya kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka la Uswidi, Ibrahimovic ambaye kwa sasa ni mchezaji wa AC Milan nchini Italia, alimtumia kocha Janne Andersson ujumbe wa kumwarifu kwamba hataweza kushiriki fainali za Euro kutokana na jeraha. Fainali hizo zimeratibiwa kuanza Juni 11 hadi Julai 11, 2021.

Ibrahimovic alipata tatizo hilo la goti akichezea AC Milan dhidi ya Juventus katika Serie A mnamo Mei 9, 2021. Aliondolewa uwanjani katika dakika ya 66 kwenye mchuano huo ambao AC Milan walishinda 3-0. Kufikia sasa, amefungia Uswidi jumla ya mabao 62 na ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa kikosi hicho.

Mnamo Machi 2021, Ibrahimovic alichangia bao katika ushindi uliosajiliwa na Uswidi dhidi ya Georgia katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar. Hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuwajibishwa katika timu ya taifa baada ya kuwa nje kwa kipindi cha miaka mitano.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

UEFA: Huenda Aguero asicheze kwenye fainali ya Machester...

Malalamiko ya ODM uchaguzi mdogo Bonchari