• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
WASONGA: Muturi asalie msemaji wa Mlimani, asiwanie urais 2022

WASONGA: Muturi asalie msemaji wa Mlimani, asiwanie urais 2022

Na CHARLES WASONGA

RIPOTI kwamba Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi atawania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 ni ithibati tosha kwamba Rais Uhuru Kenyatta hana nia ya kuliacha taifa lililo thabiti kisiasa baada ya kustaafu kwake.

Hii ni kwa sababu Wakenya kutoka maeneo mengine watahisi kusalitiwa na watu wa Mlima Kenya. Hii ni kwa sababu wengi wanaamini kuwa wakazi wa eneo hilo wanapaswa “kurudisha mkono” kwa kuunga mkono wagombea urais kutoka sehemu nyinginezo za nchi.

Watu kutoka eneo la Nyanza ambalo ni ngome ya kiongozi wa ODM Raila Odinga wamekuwa wakiamini kuwa Rais Kenyatta atamuunga mkono kigogo huyu wa siasa za eneo hili kuwa Rais, “kwa moyo wa handisheki.”

Wanasiasa wengine wanaotamani kupata baraka za kiongozi wa taifa ni kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi na waziri wa zamani wa Biashara Mukhisa Kituyi.

Hii ni kwa sababu uwezekano kwamba Rais Kenyatta atamuunga mkono Naibu wake, William Ruto, unaendelea kuwa finyu kama ilivyodhihirika juzi wakati wa Hafla ya Maombi ya Kitaifa katika majengo ya Bunge. Viongozi hao wawili walionekana wazi kukinzana kimawazo kuhusiana na masuala mbalimbali ya kitaifa.

Kwa hivyo ikiwa ni kweli, Bw Muturi atajitosa katika kinyang’anyiro cha urais alivyodokeza Gavana wa Meru Kiraitu Murungi, hatua hiyo bila shaka itasawiriwa kuwa na baraka za Rais Kenyatta. Sababu ni kwamba, kutawazwa kwa Bw Muturi kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya kulikuwa na baraka za kiongozi huyo wa taifa.

Japo naamini kujitosa kwa Bw Muturi katika kinyang’anyiro cha urais ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa jamii za Mlima Kenya zinapata usemi katika serikali ijayo, hatua hii itachangia jamii za maeneo mengine kuwachukulia kama “wenye ubinafsi wa kisiasa.”

Licha ya kuwa baadhi ya wanasiasa kutoka jamii ya Wakikuyu wanapinga kutawazwa kwa Muturi kuwa msemaji wa Mlima Kenya, mwishowe watamuunga mkono baada ya “kuona mwanga.”

Sikubaliani na wale wanaodai kuwa Bw Muturi anatoka kabila dogo la Mbeere ambalo halijawahi kutoa mgombeaji urais na kwamba ni watu kutoka jamii ya Wakikuyu ambao wamewahi kushikilia wadhifa huo.

Dhana iliyowakolea Wakenya wengi ni kwamba jamii hizi mbili pamoja na Wameru, Waembu na Watharaka ni “matawi ya mti mmoja.”

Kwa hivyo japo ni haki ya kila Mkenya, aliyehitimu, kuwania urais, watu kutoka eneo la Mlima Kenya waunge mkono wagombeaji urais kutoka kutoka sehemu nyinginezo za nchi ili kudumisha umoja wa nchi.

Muturi asalie msemaji tu wa Mlima Kenya, asiwanie urais.

You can share this post!

Watford wasajili kiungo Louza wa Nantes kadri wanavyojisuka...

Manchester City tayari kufungulia mifereji ya fedha na...