• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Manchester City tayari kufungulia mifereji ya fedha na kusajili wanasoka wa haiba kubwa muhula huu

Manchester City tayari kufungulia mifereji ya fedha na kusajili wanasoka wa haiba kubwa muhula huu

Na MASHIRIKA

MWENYEKITI wa Manchester City, Khaldoon al-Mubarak, amesema kwamba kikosi chake kiko radhi kufungulia mifereji ya fedha na kujishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho wa wachezaji muhula huu.

Kwa mujibu wa Khaldoon, Man-City wana kiu ya kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kutia kibindoni taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

“Tumeweka wazi malengo yetu. Tutahitajika kujinasia huduma za wanasoka stadi, wazoefu na mahiri zaidi ili tufaulu katika maazimio hayo,” akasema kinara huyo.

Kauli ya Khaldoon inatolewa wakati ambapo tetesi kuhusu uwezekano wa sogora Harry Kane kubanduka kambini mwa Tottenham Hotspur na kutua ugani Etihad kuvalia jezi za Man-City zinazidi kushika kasi.

“Baada ya kushinda EPL na kutinga fainali ya UEFA, huu si wakati wa kuridhika kwa kukaa chini kutulia. Kufanya hivyo ni kosa kubwa. Hiki ndicho kipindi cha kuwapa mashabiki wetu matarajio makuu zaidi kwamba kikosi hakijaridhika na mataji mawili pekee muhula huu – EPL na League Cup. Tuna kiu ya mafanikio zaidi na kuvunja rekodi nyingi iwezekanavyo,” akaongeza.

Kubwa zaidi katika malengo ya Man-City ni kusajili fowadi atakayekuwa kizibo cha mshambuliaji Sergio Aguero aliyeyoyomea Barcelona baada ya mkataba wake kambini mwa Man-City kutamatika.

“Japo hazina yetu iliathiriwa na janga la corona, bado tuna kiasi kizuri cha fedha kwa ajili ya usajili ya wachezaji matata. Tutawekeza kwa busara,” akaongeza Khaldoon.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

WASONGA: Muturi asalie msemaji wa Mlimani, asiwanie urais...

TAHARIRI: Mapuuza ni hatari kwa haki na sheria