• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
TAHARIRI: Mapuuza ni hatari kwa haki na sheria

TAHARIRI: Mapuuza ni hatari kwa haki na sheria

KITENGO CHA UHARIRI

JANA Jumanne Wakenya walipokuwa wakiadhimisha miaka 58 tangu wajipatie uhuru wa ndani, mojawapo ya mambo yaliyotazamwa kwa karibu ni orodha ya wageni waalikwa mjini Kisumu.

Kati ya wageni hao, alikuwa Bw Mohamed Abdi Mahamud, ambaye wiki mbili zilizopita aliachishwa kazi na Bunge la Seneti kama gavana wa Wajir.

Kuhudhuria shehere hizo akiwa ‘gavana’ kulitokea siku chache baada ya Bw Mahamud kuhudhuria mkutano wa Baraza la Magavana (CoG) jijini Nairobi. Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Martin Wambora (Embu) aliungana na magavana wengine kukariri kwamba walimtambua Bw Mahamud kuwa gavana halali.

Kauli hiyo kwamba kuondolewa kwa Bw Mahamud na kuapishwa kwa naibu wake Bw Ahmed Ali Mukhtar ni kinyume cha Katiba, haina msingi kisheria.

Jaji wa mahakama ya Meru alipotoa agizo la kusimamisha kujadiliwa kwa Bw Mahamud, shughuli za seneti zilikuwa zikiendelea. Isitoshe, seneti ni taasisi huru ambayo inaendesha shughuli zake kulingana na kanuni za Bunge.

Pili, maagizo kwamba naibu gavana asiapishwe, yalitolewa Bw Mukhtar akiwa ameshaapishwa na Jaji Said Chitembwe.

Kwa hivyo, kama kungekuwa na pingamizi yoyote, jambo la busara lingekuwa kupeleka rufaa katika Mahakama ya Rufaa. Bw Wambora anaelewa njia hizo, ikizingatiwa yeye mwenyewe amewahi kuondolewa na Seneti mara kadhaa lakini akafuata sheria na akarejeshwa.

Jambo linalohuzunisha ni kwamba, magavana wanamtetea Bw Mahamud lengo likiwa kujilinda dhidi ya kuchukuliwa hatua siku za usoni.

Kwa kuendelea kushikilia kwamba Bw Mahamud angali gavana, magavana hao wanaonyesha hawatambui wajibu wa Seneti iliopewa na Katiba. Wanajifanya kumhurumia mwenzao kwa vile wanajua kuna magavana kadhaa wanaoandamwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), kuhusu utumizi mbaya wa afisi.

Mtindo huu si mzuri kwa utekelezaji wa sheria nchini. Kama kila mwenye mamlaka ataruhusiwa apuuze taasisi zetu, basi nchi yetu itageuka jangwa lenye ‘mwenye nguvu mpishe’.

Kuruhusu watu kupuuza uamuzi wa seneti na kuapishwa na naibu gavana kuna maana moja tu. Kwamba nchi hii kila mtu afanye apendavyo bila kujali haki na sheria. Hii ni hatari.

You can share this post!

Manchester City tayari kufungulia mifereji ya fedha na...

GWIJI WA WIKI: Dkt Naomi Musembi