• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Vuguvugu la Linda Katiba halitachoka kunusuru nchi – Karua

Vuguvugu la Linda Katiba halitachoka kunusuru nchi – Karua

Na SAMMY WAWERU

SIEGEMEI upande wowote wa kisiasa katika mchakato wa Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), amesema Bi Martha Karua.

Kiongozi huyo wa Narc-Kenya amesema mrengo anaoegemea ni ule wa kuokoa Katiba ya Kenya, chini ya vuguvugu la Linda Katiba analoongoza.

“Mirengo kadha imechipuka, kuna inayounga mkono, mingine kupinga kwa sababu za ushawishi wa kisiasa. Mimi ninasimama na mrengo unaofuata sheria kuokoa Katiba – Linda Katiba,” Bi Karua akasema.

Licha ya mahakama kuu kuharamisha BBI, mswada maarufu unaopendekeza Katiba kufanyiwa marekebisho, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga na ambao ni waasisi, wamekata rufaa uamuzi huo.

Mahakama ya rufaa jana ilitangaza kuwa kesi hiyo itasikilizwa kati ya Juni 29 na Julai 2, 2021.

Aidha, itasikilizwa na jopo la majaji saba, wakiongozwa na jaji mkuu wa mahakama ya rufaa, Bw Daniel Musinga.

Wakati ikifutilia mbali, mahakama kuu ilitaja BBI kama mswada haramu, na ambao haukuzingatia sheria za Katiba kuuanzisha.

Mengi ya mabunge ya kaunti, la kitaifa na pia seneti, yaliuidhinisha.

Mahakama kuu ilisisitiza marekebisho ya Katiba yanapaswa kuanzishwa na Mkenya binafsi au kundi la Wakenya binafsi, ila si asasi ya serikali.

“Sheria imeweka wazi kuhusu mchakato wa marekebisho ya Katiba. Linda Katiba itaendelea kusimamia ukweli,” Karua ambaye pia ni wakili akasisitiza.

Bi Karua pia anapendekeza fedha ambazo zitatumika kukata rufaa, zielekezwe kukabili virusi vya corona na kukwamua uchumi.

You can share this post!

LISHE: Rosti ya maini

Wanafunzi wa kike kunufaika na ufadhili wa sodo