• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
MATHEKA: Rais hakufaa kutumia sherehe kutishia mahakama

MATHEKA: Rais hakufaa kutumia sherehe kutishia mahakama

Na BENSON MATHEKA

KAULI ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba Mahakama imemsukuma hadi ukutani ni hatari hasa kutoka kwa kiongozi wa nchi.

Ni hatari hasa kwa vile amekuwa akionyesha kutoridhishwa na uhuru wa majaji katika kuamua kesi zinazowasilishwa mbele yao wasipokubaliana na serikali.

Ni tamko ambalo linaweza kuchochea umma dhidi ya mahakama ambayo inatekeleza majukumu yake ya kikatiba.

Japo rais ana haki ya kutofurahishwa na uamuzi dhidi yake, hakufaa kutumia hafla ya kitaifa kushutumu idara hiyo na majaji kwa kutekeleza majukumu yao.

Hii inaweza kuchochea wafuasi wake dhidi ya mahakama na kuweka utawala wa sheria ambao nchi hii imekumbatia kwa miaka mingi kwenye hatari.

Kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya sherehe za Madaraka Dei na siku moja kabla ya Mahakama ya Rufaa kuanza vikao vya kusikiliza rufaa ambayo amekata pamoja na washtakiwa wengine dhidi ya uamuzi ulioweka breki mchakato wa kubadilisha katiba, inaweza kuchukuliwa kama vitisho kwa majaji watakaosikiliza rufaa hiyo.

Kwa kusema kwamba mahakama imesukuma serikali yake hadi ukutani hasa kuhusu suala la BBI, ni kumaanisha kwamba hayuko tayari kuachana na mchakato huo hata kama rufaa yake haitafaulu. Ukweli ambao wanaolaumu mahakama wanapuuza, ni kuwa ni taasisi ya kikatiba ilivyo serikali kuu, bunge na tume nyingine za kikatiba na uhuru wake umehakikishwa na katiba hiyo.

Rais aliapa kulinda katiba hiyo na kuiheshimu kila wakati na alichopaswa kufanya ni kusubiri mfumo wa haki ambao ameanza kutumia kwa kukataa rufaa ukamilike.

Kufanya hivi, ni kuonyesha mfano wa kuigwa na raia wote na kuheshimu katiba ambayo aliapa mbele ya Wakenya wote.

Iwapo mchakato wa kubadilisha katiba wa BBI ni wa wananchi waasisi wake wanavyosisitiza, ni wananchi wenyewe walioweka mahakama katika katiba walipokubali utawala wa demokrasia.

Kwa sababu ya uhuru iliyotwikwa na katiba, mahakama imekuwa ikitoa maamuzi ya kulinda mwananchi wa kawaida dhidi ya hatua kadamizi za serikali na kufuatia kauli za maafisa wa serikali, hawafurahishwi na uhuru huu.

Haki haiwezi kuwa ni wakati mahakama inakubaliana na serikali lakini inapokosa kufanya hivyo. Kumbukumbu kuu ambayo Rais Kenyatta ataachia Wakenya inafaa kuwa kuheshimu utawala wa sheria unaojumuisha uhuru wa mahakama na sio kubadilisha katiba.

You can share this post!

WASONGA: Upimaji corona Kisumu uanzishwe mara moja!

UMBEA: Siku hizi makahaba hawapo tena barabarani, wapo...