• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
KAMAU: Uongozi bora ndio wenzo wa kufuta dhuluma za tangu jadi

KAMAU: Uongozi bora ndio wenzo wa kufuta dhuluma za tangu jadi

Na WANDERI KAMAU

MIEZI minne baada ya mauaji ya mwanasiasa Tom Mboya mnamo Julai 5, 1969, Mzee Jomo Kenyatta alifanya ziara ya siku mbili jijini Kisumu kufungua Hospitali ya New Nyanza.

Wakati huo, kulikuwa na taharuki kubwa ya kisiasa katika eneo la Luo Nyanza.

Jamii ya Waluo ilihisi serikali ya Mzee Kenyatta ilikuwa na mkono fiche kwenye mauaji ya Mboya.

Hali hiyo ilizidishwa na uhusiano mbaya uliokuwepo kati ya Mzee Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga, baada ya Jaramogi kufurushwa kutoka Kanu.

Ilimlazimu Jaramogi na wabunge kadhaa kutoka eneo hilo kujiuzulu kutoka Kanu na kuchaguliwa tena kupitia chama cha Kenya Peoples’ Union (KPU).

Licha ya mazingira hayo magumu, Mzee Kenyatta hakuonekana kutishwa na aina ya mapokezi ambayo angepata kutoka kwa wenyeji. Lengo lake lilikuwa kudhihirisha yeye ndiye bado alikuwa rais.

Hata hivyo, hali iligeuka na kuwa tandabelua.

Wenyeji hawakutaka kusikia lolote kumhusu Mzee Kenyatta wala serikali yake. Kile walichotaka tu ni haki ya ‘mwana wao’ Mboya.

Kizaazaa kilizuka. Wenyeji wakaanza maandamano kuonyesha kutoridhishwa kwao na Mzee Kenyatta.

Kwenye patashika hiyo, ilibidi polisi na walinzi wa Rais kufyatua risasi ili kutuliza hali.

Kulingana na takwimu za serikali, watu 11 waliuawa ijapokuwa baadhi ya ripoti zimekuwa zikidai kuwa karibu watu 100 walipoteza maisha yao.

Tukio hilo ndilo liliweka msingi kwa uhusiano mbaya wa kisiasa ambao umekuwepo kati ya marais wa awali nchini na wenyeji wa eneo la Nyanza.

Hali hiyo ilidorora wakati wa tawala za Rais Mstaafu Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, ikizingatiwa wanatoka katika eneo la Kati.

Hata hivyo, taswira iliyojitokeza Jumanne jijini Kisumu wakati wa sherehe za Sikukuu ya Madaraka, inadhihirisha uongozi mzuri ndiyo njia ya kufuta dhuluma za kijadi ambazo zimeyakumba maeneo mbalimbali nchini.

Kinyume na awali, wenyeji walisahau tofauti za kisiasa na kuwapokea vyema Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto, licha ya wawili hao kuwa washindani wakali wa kisiasa wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Baada ya uchaguzi mkuu tata wa 2017, Rais Kenyatta na Dkt Ruto walionekana kama “maadui” wa kisiasa wa ukanda huo.

Hata hivyo, mapokezi ya kipekee waliyopokea viongozi hao wawili yanaonyesha kuwa uongozi ufaao ndiyo funguo ya kuiponya nchi dhidi ya makovu yote ya kisiasa na kikabila yaliyotokea katika miaka ya nyuma.

[email protected]

You can share this post!

Wazee watakasa madhabahu ya Agikuyu

MUTUA: Huenda Museveni ana nia mbovu inayoleta maafa