• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
MUTUA: Huenda Museveni ana nia mbovu inayoleta maafa

MUTUA: Huenda Museveni ana nia mbovu inayoleta maafa

Na DOUGLAS MUTUA

JARIBIO la kumuua mmoja kati ya wanajeshi na mawaziri maarufu zaidi nchini Uganda siku chache zilizopita limewaacha wengi vinywa wazi wasiwe na la kusema.

Maswali nayo yanaulizwa kwa kunong’onezana kwa kuwa Jenerali Edward Katumba Wamala si mtu wa kawaida.

Nayo hiyo ni nchi ya Jenerali Yoweri Kaguta Museveni, kidomodomo kinaweza kukutia pabaya ukajuta kuzaliwa.

Hata hivyo, ni lazima watu waulizane maswali: Je, ni tukio la ugaidi? Huenda magaidi wa al-Shabaab wamejaribu kulipiza kisasi baada ya wenzao kusagwa na Museveni kama unga?

Kumbuka walioshukiwa kushambulia Uganda wakati wa fainali za Kombe la Dunia la kabumbu mnamo 2010 waliponea kunyongwa, wakafungwa jela muda mrefu.

Au labda jaribio la kumuua jenerali wa watu ni zao la siasa za urithi ambazo zimeendelea kwa muda sasa? Mzee Museveni akiondoka leo hii, wa kumrithi ni nani?

Labda Jenerali Katumba Wamala ni mmoja wa watu wanaotarajiwa kumpa ushindani mwanawe Museveni, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba?

Au pengine hata ni jaribio la waasi wanaojiita Allied Democratic Forces (ADC) kutangaza kuwa wangali ngangari kukabiliana na serikali ya Uganda?

Gari lililombeba Jenerali Wamala lilishambuliwa kwa risasi 50 mnamo Jumanne. Milipuko ya risasi hizo ilipokoma, binti yake, Brenda Nantongo, alikuwa keshauawa. Dereva wa waziri huyo pia kwa jina Haruna hakunusurika.

Manusura wa pekee walikuwa Jenerali na mlinzi wake, Sajini Khalid Koboyoit, ambaye sasa ni shujaa wa kitaifa kwa kujitoa kama ngao ili kumwokoa mkuu wake wa kazi.

Akimpa pole kwa njia ya simu muda mfupi baadaye, Rais Museveni alimwambia Jenerali Wamala kwamba tayari waliomshambulia wanajulikana na wangeandamwa.

Hivi huyu Jenerali Wamala ni nani? Kama mshirika wa karibu wa Rais Museveni, ana rekodi ya kipekee ya kuwahi kuwa mkuu wa polisi na pia mkuu wa majeshi.

Jenerali huyo aliyesoma Marekani na vyuo vingine vya kijeshi maarufu duniani alikuwa mwanajeshi wa kwanza kutumika kama Inspekta Mkuu wa Polisi kati ya mwaka 2001 na 2005.

Baadaye alipata nyadhifa kadhaa kisha akateuliwa Mkuu wa Majeshi mnamo 2013, akahudumu hadi alipostaafu mnamo 2017, akajiunga na siasa na kuteuliwa waziri.

Alistaafishwa wakati ambapo minong’ono ilipamba moto kwenye jeshi la Uganda kuhusu kile kilichoaminiwa kuwa juhudi za Rais Museveni kumwandaa mwanawe kumrithi.

Iliaminika kwamba hata uteuzi wake wa kuliongoza jeshi ilikuwa mbinu ya kuwasahaulisha Waganda kuhusu sakata ya urithi iliyofichuliwa na jenerali mwingine wa jeshi hilo.

Wakati huo, Jenerali David Sejusa alimwandikia barua mkuu wa majasusi akipendekeza uchunguzi ufanywe kuhusu madai ya kuwapo mpango wa kuwaua majenerali waliopinga juhudi za kumrithisha urais Kainerugaba.

Ukizingatia umaarufu wa Jenerali Wamala na uzoefu wake wa kazi, basi unasalitika kuwaelewa wanaoshuku kwamba huenda alilengwa kutokana na siasa za urithi.

Inaaminika kuwa Rais Museveni ameaminia kumpa usukani mwanawe, ambaye sasa ni kamanda wa vikosi maalumu jeshini.

Kuhusu uwezekano kwamba magaidi ndio waliomshambulia Jenerali Wamala, inatambuliwa kuwa watu 36 wameuawa katika hali za kutatanisha tangu 2010.

Bi Joan Kagezi, mkuu wa mashtaka katika kesi ya washukiwa wa mashambulio hayo ya kigaidi ya 2010, aliuawa mnamo 2015.

Msemaji wa Polisi, Bw Andrew Felix Kaweesi, aliyeuawa mnamo 2017, ni miongoni mwa maafisa wa usalama, ulinzi na viongozi wa kidini walioangamizwa hivyo.

Tayari ni kosa kubwa kwa Museveni kutaka kumrithisha mwanawe uongozi wa nchi, lakini atakosea maradufu iwapo juhudi zake hizo zitasababisha usalama wa kitaifa kuzorota.

Raia wa Uganda wanaolipa ushuru wanapaswa kuhakikishiwa usalama wao, iwe ni wakati wa mikakati ya kisiasa au mapambano dhidi ya jinai hatari kama ugaidi.

[email protected]

You can share this post!

KAMAU: Uongozi bora ndio wenzo wa kufuta dhuluma za tangu...

Uhuru akaa ngumu majaji wakilia