• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Gerrard na Benitez kati ya wakufunzi sita wanaomezea mate mikoba ya Everton

Gerrard na Benitez kati ya wakufunzi sita wanaomezea mate mikoba ya Everton

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

STEVEN Gerrard na Rafa Benitez ni miongoni mwa wakufunzi sita ambao Everton wamefichua kwamba wanawania nafasi ya kujaza nafasi iliyoachwa wazi na kocha Carlo Ancelotti uwanjani Goodison Park.

Kwa mujibu wa gazeti la Athletic nchini Uingereza, Everton almaarufu ‘The Toffees’ wanatarajiwa kumtangaza mkufunzi mpya chini ya kipindi cha wiki moja ijayo kwa minajili ya kuanza kazi ya kukiandaa kikosi kwa kampeni za msimu mpya wa 2021-21.

Ancelotti alikatiza ghalfa uhusiano wake na Everton wiki hii na kurejea Real Madrid kudhibiti mikoba iliyoachwa na kocha Zinedine Zidane aliyejiuzulu baada ya miamba hao wa Uhispania kukamilisha kampeni za muhula wa 2020-21 bila taji lolote kwa mara ya kwanza tangu 2009-10.

Yalikuwa matarajio ya Everton kujisuka upya msimu huu chini ya Ancelotti kwa maazimio ya kuwa miongoni mwa wawaniaji halisi wa nafasi nne za kwanza kileleni mwa jedwali la EPL mnamo 2021-22 na hivyo kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2022-23.

Gerrard aliowaongoza waajiri wake wa sasa, Rangers kutia kapuni taji la Ligi Kuu ya Scotland msimu wa 2020-21 bila kupoteza hata mechi moja.

Akipigiwa upatu wa kuwa mrithi wa kocha Jurgen Klopp kambini mwa Liverpool hatimaye, huenda Gerrard akashawishika zaidi kutua jijini Merseyside kudhibiti mikoba ya Everton ili kupata uzoefu utakaomfaa zaidi katika ulingo wa ukufunzi.

Benitez aliwahi kudhibiti mikoba ya Liverpool na aliwaongoza miamba hao kutia kapuni taji la UEFA mnamo 2006.

Kocha huyo raia wa Uhispania aliyewahi kuwatia makali masogora wa Newcastle United kati ya 2016 na 2019, bado hajaajiriwa na kikosi chochote tangu abanduke kambini mwa Dalian Pro nchini China mnamo Januari 2021.

Mbali na Gerrard na Benitez, wakufunzi wengine wanaohusishwa na mikoba ya Everton ni David Moyes wa West Ham United, Roberto Martinez wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Erik ten Hag wa Ajax na kocha wa zamani wa Wolves, Nuno Espirito Santo.

  • Tags

You can share this post!

Stoke City warefusha mkataba wa kiungo Obi Mikel kwa mwaka...

Mkimbizi Msafiri akimbia kilomita zaidi ya kilomita 500...