• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Uhispania na Uswidi waumiza nyasi bure kwenye kipute cha Euro

Uhispania na Uswidi waumiza nyasi bure kwenye kipute cha Euro

Na MASHIRIKA

LICHA ya Uhispania kutamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira uwanjani, kikosi hicho cha kocha Luis Enrique bado kiliambua sare tasa dhidi ya Uswidi katika mchuano wa Kundi E kwenye fainali za Euro mnamo Jumatatu usiku jijini Seville.

Uhispania waliotawazwa mabingwa wa Euro mnamo 2012 baada ya kushinda Kombe la Dunia mnamo 2010, walipoteza nafasi nyingi za wazi katika vipindi vyote viwili vya mchezo licha ya kukamilisha jumla ya pasi 419 katika kipindi cha kwanza.

Alvaro Morata alikuwa mwiba kwa beki Marcus Danielson wa Uswidi huku ushirikiano wake na Dani Olmo pamoja na Jorge Koke ukimtatiza pakubwa kipa Robin Olsen.

Fursa ya pekee ya kufunga bao ambayo Uswidi walipata ni kupitia chipukizi Alexander Isak aliyemwelekezea kipa Unai Simon kombora zito mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Isak alionana sana na Marcus Berg katika safu ya mbele ya Uswidi.

Sare tasa ambayo Uhispania walilazimishiwa na Uswidi ina maana kwamba Slovakia wanadhibiti sasa kilele cha Kundi E kwa alama tatu baada ya kuwakung’uta Poland 2-1 mapema Jumatatu.

Maandalizi ya Uhispania kwa fainali za Euro mwaka huu yalivurugwa katika dakika za mwisho baada ya nahodha Sergio Busquets na beki Diego Llorente kuugua Covid-19.

Aidha, kocha Enrique aliduwaza mashabiki wengi kwa kumtupa nje beki matata wa Real Madrid, Sergio Ramos, 35, kwenye kikosi chake cha Euro.

Ramos amekuwa mkekani kwa kipindi kirefu katika msimu wa 2020-21 akiuguza jeraha na amechezea waajiri wake mara moja pekee tangu mwisho wa Machi 2021.

Kutokuwepo kwa Ramos katika kikosi cha Uhispania sasa kunamaanisha kwamba hakuna mwanasoka yeyote kutoka klabu ya Real ambaye anashiriki soka ya Euro mwaka huu akivalia jezi za Uhispania ambao pia walitwaa ubingwa wa Euro mnamo 2008.

Ramos aliwajibishwa na Uhispania mara ya mwisho mnamo Machi 2021 katika mechi za kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar. Alitokea benchi katika sare dhidi ya Ugiriki kabla ya kutokea benchi kwa mara nyingine katika ushindi dhidi ya Kosovo.

Enrique aliteua kumpanga Morata anayejivunia mabao 19 kimataifa katika kikosi chake cha kwanza na kumwacha nje fowadi Gerard Moreno aliyefungia Villarreal jumla ya mabao 30 katika msimu wa 2020-21 kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Uswidi kwa sasa watamenyana na Slovakia katika jiji la Saint Petersburg nchini Urusi mnamo Juni 18, siku moja kabal ya Uhispania kupepetana na Poland jijini Seville.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Sheria za mashabiki kujiweka salama Safari Rally zatangazwa

Ukambani nao wafuata minofu Ikulu