• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wanafunzi watatu wa Thika School for the Blind ni wajawazito

Wanafunzi watatu wa Thika School for the Blind ni wajawazito

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuwalinda wanafunzi walemavu hasa wasioona ili kuwaepusha na changamoto wanazopitia.

Afisa mkuu wa idara ya watoto kaunti ndogo ya Thika, Bi Dinnah Mwangi, amesikitika kuwa tayari kuna kesi tatu za wasichana wa shule ya upili ya Thika School for the blind, ambao ni wajawazito huku wakitarajia kujifungua hivi karibuni.

Kulingana na afisa huyo, wanafunzi hao wenye ulemavu wa kuona walibakwa na watu wasiowajua walipokuwa likizoni.

Alieleza kuwa wanafunzi wengi walemavu wanapitia masaibu mengi jambo ambalo linastahili kuchunguzwa na serikali.

Alitoa wito kwa serikali kuwaadhibu watu wanaovizia walemavu ili kuwadhulumu kimapenzi.

Aliyasema hayo akiwa katika shule ya Thika School for the blind Jumatano wakati wa kuadhimisha siku ya watoto nchini.

Aliiomba serikali kuingilia kati kuona ya kwamba wanafunzi walemavu wanashughulikiwa kwa njia ifaayo.

Alitoa wito kwa serikali kusambaza vifaa vya kisasa vya masomo katika shule za wanafunzi walemavu ili wawe na nafasi bora kama wale wa kawaida.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanafunzi wapatao 400 ambao wengi wao walitoa wito kwa serikali kuwapa vifaa bora vya masomo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi Margaret Karera alikiri kuwa kuna changamoto tele kwa walimu hasa wakati huu wa homa ya Covid-19.

“Wanafunzi walemavu wanapobaki peke yao katika mabweni huwa ni vigumu sana kuwafuatilia iwapo wanaweka nafasi miongoni mwao. Ni muhimu kuwafuatilia kwa karibu kila mara,” alisema Bi Karera.

Aliitaka serikali kusambaza vifaa bora vya kisasa ambavyo vitaambatana na masomo yao kwa wakati huu.

Aliitaka serikali kuwapa nafasi sawa wanafunzi walemavu na wale wa kawaida ili wote wasajili matokeo bora bila vizingiti.

You can share this post!

Magari matatu ya Sh13 milioni kila moja kutumiwa na...

Kiungo Eriksen ahakikishia mashabiki kuwa hali yake sasa ni...