• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Vinara wa NASA wawakanganya wafuasi wao

Vinara wa NASA wawakanganya wafuasi wao

BENSON MATHEKA Na PIUS MAUNDU

LAWAMA ambazo vinara wa muungano wa NASA wanarushiana kuhusu mkataba wa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 zimeacha wafuasi wao wakijiuliza ni nani kati yao anayesema ukweli.

Muungano huo unashirikisha vyama vya ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, Wiper cha Kalonzo Musyoka, Ford Kenya kinachoongozwa na Moses Wetangula na Amani National Congress kinachoongozwa na Musalia Mudavadi.

Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula wamekuwa wakimlaumu Bw Odinga kwa kukiuka mkataba huo kwa kukataa kuunga mmoja wao kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kulingana na wanasiasa hao, walikubaliana kuwa wangemuunga Bw Odinga kugombea urais kwenye uchaguzi wa 2017 na kisha aunge kinara mwenza kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Vinara hao wanasema kwamba Bw Odinga alikubali kumuunga Bw Musyoka au Bw Mudavadi lakini waziri huyo mkuu wa zamani, maafisa na wabunge wa chama chake wamekuwa wakikanusha madai hayo.

Wanasisitiza kuwa ahadi hiyo ilipaswa kudumu iwapo Bw Odinga angeshinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Ingawa Bw Odinga hajatangaza iwapo atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, wandani wake wamekuwa wakimpigia debe kwa urais.

Hata hivyo, Bw Musyoka na Bw Mudavadi wanasisitiza kuwa ODM ilikaidi mkataba huo na hawako tayari kumuunga mkono Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu ujao.Jana, Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana alimtetea Bw Odinga akisema kwamba mkataba huo ungetekelezwa iwapo NASA ingeshinda urais na kuunda serikali.

Alikiri kwamba kulingana na mkataba huo Bw Odinga angemuunga mkono Bw Musyoka kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 kama angeshinda urais.

“Mimi na Makau Mutua tulikuwa mashahidi wa mkataba kati ya Raila Odinga na Kalonzo Musyoka ulioeleza kuwa Raila angemuunga Kalonzo 2022 iwapo NASA ingeshinda 2017 na muungano huo ungebabaki imara hadi 2022. Awali, vinara watano wa NASA walikuwa wametia saini mkataba wa maelewano kwamba Raila angeunga mmoja wa vinara wenza iwapo angeshinda urais,” alisema Bw Kibwana kupitia ujumbe wa Twitter.

Bw Kibwana ambaye alikuwa mshirika wa Bw Musyoka alikuwa shahidi wa mkataba ambao makamu rais huyo wa zamani alikubali kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 chini ya muungano wa NASA.

Kulingana na Bw Kibwana, Odinga alikuwa ametia saini mkataba mwingine na vinara wenza wa muungano huo ambao haukumtaka kiongozi huyo wa ODM kumuunga Bw Musyoka moja kwa moja kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.Mnamo 2017 katika mkutano wa NASA uliofanyika katika uwanja wa Machakos Golf Club, Bw Kibwana alimtaka Bw Odinga kuheshimu mkataba wake na kumuunga Bw Musyoka kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wakati huo, Bw Odinga alimjibu kwamba walikuwa bado mawindoni kwa kuwa hawakuwa wameshinda urais walivyotarajia.

“Mnyama tuliyewinda alituponyoka na hatuna nyama ya kugawana. Profesa, wacha tufukuze mnyama kwanza,” alisema Bw Odinga katika mkutano uliohudhuriwa na Bw Mudavadi na Bw Wetangula na washirika wao.

Kulingana na Bw Mudavadi, Bw Odinga na chama chake cha ODM kiliwasaliti washirika wake katika NASA na hawezi kuaminiwa.

You can share this post!

Wapwani si wavivu, Shahbal asema

JAMVI: Madhara yanukia IEBC ikibanwa na muda wa maandalizi...