• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:58 PM
TAHARIRI: Viongozi wasiijadili kesi ya rufaa ya BBI

TAHARIRI: Viongozi wasiijadili kesi ya rufaa ya BBI

KITENGO CHA UHARIRI

MAHAKAMA ya Rufaa inapoanza kusikiliza kesi kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) hii leo, itakuwa busara kwa wanasiasa na pande zinazohusika kutoijadili nje ya Mahakama.

Tangu Majaji watano wa Mahakama Kuu walipositisha mchakato huo, kumekuwa na mihemko huku hisia na maoni mbali mbali yakitolewa kwenye vyombo vya habari na katika mikutano ya hadhara.

Ni kawaida ya kukosoa uamuzi wa majaji hao lakini sasa, kwa kuwa kesi imeanza, itakuwa busara kwa viongozi wa kisiasa kuheshimu utawala wa kisheria na kuwapatia majaji fursa ya kusikiliza na kufanya uamuzi wao.

Waliokata rufaa wanaamini kwamba wako na sababu za kutosha za kukosoa uamuzi wa majaji lakini kuzizungumzia nje ya mahakama hakutafaa kesi yao. Kwa hakika, kufanya hivyo kuna hatari chungu nzima.

Vile vile, waliowasilisha kesi katika Mahakama Kuu iliyosababisha mchakato huo kusitishwa, wanaamini kwamba wana sababu za kushawishi majaji saba wa Mahakama ya Rufaa kuidhinisha uamuzi wa majaji watano wa Mahakama Kuu.

Kutoa matamshi kuhusu kesi hiyo katika majukwaa mengine mbali na mbele ya majaji ni sawa na kutaka kuyumbisha mkondo wa haki, kuchochea umma na ni ukiukaji wa sheria na kanuni za mahakama.

Sio vyema kwa viongozi walioapa kulinda, kutetea na kuheshimu utawala wa sheria kuwa msitari wa mbele kuupuuza.

Tunakumbusha kila kiongozi kwamba tunaelekea katika msimu wa siasa za uchaguzi mkuu wa 2022 ambapo joto la siasa huwa limepanda na matamshi anayotoa kila mmoja yanaweza kuathiri utengamano nchini.

Mawakili wa pande zote wanafaa kutayarisha wateja wao kwamba matokeo ya kesi yanaweza kuwapendelea au kupendelea upande mwingine na la busara ni kufuata mkondo wa kisheria na kwenda katika Mahakama ya Juu.

Kesi inafaa kufanyiwa ndani ya korti na kwa kufanya hivi, tutajenga nchi inayoongozwa na utawala wa kisheria.

Uamuzi unapotolewa ni vyema kusherehekea lakini hiyo haifai kuwa jukwaa la kushambulia majaji jinsi ambavyo tumekuwa tukishuhudia katika baadhi ya kesi zinazofuatiliwa kwa karibu na umma.

Viongozi wanapoonyesha busara, wataheshimika na nchi kuheshimika kwa kuruhusu utawala wa sheria kunawiri.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Wanasiasa lawamani kwa kuwapa vijana...

TSC yafungua roho kwa Knut baada ya Sossion kuondoka