• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
TAHARIRI: Vyama vya kisiasa viwe na ukomavu

TAHARIRI: Vyama vya kisiasa viwe na ukomavu

KITENGO CHA UHARIRI

HUKU uchaguzi mkuu ukiendelea kukaribia, wanasiasa na wanachama wa vyama vyao mbalimbali wanaendelea kujiandaa vilivyo kwa ajili ya shughuli hiyo ya mwaka 2022.

Huku haya maandalizi yakiendelea kutekelezwa kupitia usajili, ukosefu wa nidhamu umeripotiwa ambapo baadhi ya wanachama wa vyama fulani wamejipata wakiwa wamesajiliwa tayari katika vyama tofauti na vyao bila idhini yao. Jambo kama hili linaenda kinyume na sheria zinazotawala usimamizi wa vyama vya kisiasa nchini.

Hivi majuzi, kuliripotiwa madai kwamba wafuasi wa mojawapo wa vyama vikuu nchini walichoma mabango ya wawaniaji wa chama pinzani katika eneobunge ambapo uchaguzi mdogo unatarajiwa kufanyika mwezi huu. Ushindani wa aina hii unaenda kinyume na maadili ya uongozi.

Kutokana na ushindano huu mkubwa humu nchini, vinara kadhaa wa vyama wamekuwa wakiendesha propaganda dhidi ya wenzao wa nia ya kuwaharibia sifa ndipo wao waonekane bora zaidi huku wapinzani wao wakionekana wabaya. Vinara hawa wamekuwa wakikutana kisiri katika juhudi za kuunda miungano ya kisiasa inayolenga kushinda uchaguzi mkuu ujao.

Bila shaka vikao hivi vya kisiri vidhihirisha wazi kiwango fulani cha usaliti, unafiki na kutoaminiana kati ya viongozi hao na wafuasi wao. Hali hii ndio inachangia pakubwa uhasama kati ya wafuasi wa chama kimoja hadi kingine.

Itakuwa jambo la busara endapo vinara wa vyama hivi wataonyesha mifano bora kwa wafuasi wao hasa kudhihirisha ukomavu na uwazi wa hali ya juu katika utendakazi wao vyamani. Pia wanafaa kuonyesha ubinadamu kwa kuwajali wanachama wao.

Hatua ya Chama cha ODM kuondoa ada ya Sh100 kwa wanachana wapya wanaotaka kujisali ni ya kupongezwa. Hata ingawa inaweza kuonekana kama mbinu ya kuvutia wafuasi wengi upande wao, ni dhahiri kwamba hali ya uchumi wakati huu wa janga la Covid-19 imelemaza wengi wasiweze kugharimia mahitaji kama haya. Mbali na kitendo hicho cha ubinadamu, wakati ni huu ambapo vyama vyote nchini vinafaa kuonyesha matendo yanayodhihirisha maadili bora.

Ukosefu wa uongozi bora kutoka kwa vinara wa vyama umesababisha hali ya vyama kuundwa na kuvunjwa kila baada ya uchaguzi. Wanasiasa wa Kenya wanafaa kuiga nchi jirani Tanzania na Uganda ambapo vyama vya zamani bado viko hai na vinaendelea kunawiri. Baadhi ya nchi zingine za kuigwa barani Afrika ni kama Afrika Kusini ambayo imekuwa na chama kimoja tangu kupata uhuru wake.

You can share this post!

Moto wateketeza afisi ya naibu kamishna Lari, nyumba za...

KAMAU: Himaya za kifalme hazina nafasi sasa