• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Brazil wakomoa Chile na kuingia nusu-fainali za Copa America

Brazil wakomoa Chile na kuingia nusu-fainali za Copa America

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi Brazil walitinga nusu-fainali za Copa America baada ya kuwapokeza Chile kichapo cha 1-0 mnamo Ijumaa usiku katika uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro.

Lucas Paqueta alitokea benchi na kufungia Brazil bao la pekee na la ushindi katika dakika ya 46 kwenye mchuano huo. Brazil kwa sasa watavaana na Peru kwenye nusu-fainali mnamo Julai 6 ugani Nilton Santos jijini Rio.

Peru walifuzu kwa nusu-fainali baada ya kubandua Paraguay 4-3 kupitia mikwaju ya penalti. Vikosi hivyo viliambulia sare ya 3-3 kufikia mwisho wa muda wa ziada.

Goli la Brazil dhidi ya Chile lilijazwa kimiani dakika mbili pekee kabla ya fowadi wa Brazil, Gabriel Jesus kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumkabili visivyo kiungo mkabaji wa Chile, Eugenio Mena.

Neymar Jr na kocha wa Brazil, Adenor ‘Tite’ Bacchi walisema kwamba tukio hilo katika ya Jesus na Mena lilikuwa “ajali ya kawaida” katika soka kwa sababu Jesus ambaye ni mshambuliaji wa Manchester City, hakuwa amemwona mpinzani wake huyo alipowania mpira wa juu kwa kutumia miguu.

Japo kupunguzwa kwa wanasoka wa Brazil kuliwapa Chile motisha tele ya kuvamia lango la wapinzani wao, mabeki wa Brazil walisalia imara.

“Ilitulazimu kujitahidi maradufu na kuvuruga mipango yote ya Chile kila walipokaribia kijisanduku chetu. Nashukuru kwamba tulisalia imara na kila mmoja akamakinikia majukumu yake ugani,” akasema beki Thiago Silva ambaye hucheza soka ya kulipwa kambini mwa Chelsea, Uingereza.

Paqueta aliletwa ugani katika kipindi cha pili kujaza nafasi ya Roberto Firmino ambaye pia alimshughulisha vilivyo kipa Claudio Bravo wa Chile. Licha ya ujio wake kuongeza kasi ya mchezo, Chile ndio walipata nafasi nyingi zaidi za kufunga kupitia Eduardo Vargas na Ben Brereton.

“Mechi dhidi ya Chile ilikuwa kipimo kamili cha uthabiti wetu. Nasi tulidhihirisha kwamba tuna nguvu za kuhimili ushindani mkubwa katika kila hali. Kubwa zaidi katika malengo yetu ni kuhifadhi ufalme wa Copa America,” akasema Neymar.

Kiungo Arturo Vidal wa Chile kwa upande wake alisema kwamba ilikuwa tija na fahari kuaga kipute cha Copa America kifalme.

“Tulipoteza dhidi ya timu inayopigiwa upatu kuhifadhi ubingwa mbele ya mashabiki wao wa nyumbani. Sasa malengo yetu ni kujinyanyua upesi na kuelekeza makini kwa mechi za kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia mnamo 2022 nchini Qatar,” akasema kiungo huyo wa zamani wa Barcelona, Bayern Munich na Juventus.

Brazil na Peru waliwahi kukutana kwenye fainali ya Copa America mnamo 2019 na wenyeji Brazil wakasajili ushindi wa 3-1.

Fainali ya Copa America mwaka huu itachezewa uwanjani Maracana mnamo Julai 10, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mourinho atua Italia kuanza kazi ya ukocha kambini mwa AS...

NDONDI: Nahodha Nick ‘Commander’ Okoth kuongoza...