• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
NDONDI: Nahodha Nick ‘Commander’ Okoth kuongoza kikosi kusaka ushindi Olimpiki

NDONDI: Nahodha Nick ‘Commander’ Okoth kuongoza kikosi kusaka ushindi Olimpiki

Na CHARLES ONGADI

NAHODHA wa timu ya taifa ya ndondi Nick ‘Commander’ Okoth ameahidi atawaongoza vyema wenzake kuvuna ushindi katika michezo ya Olimpiki nchini Japan.

Akizungumza na Taifa Leo, Okoth amesema amejiandaa vya kutosha kupeperusha bendera ya taifa katika mashindano hayo na wala haoni kizuizi cha wao kutovuna medali.

“Ninatafuta ushindi kupitia mazoezi yatakayoniwezesha kuwaongoza wenzangu kwa ushindi nchini Japan,” akasema Okoth ambaye ni bondia madhubuti wa timu ya taifa.

Okoth amepongeza benchi la ufundi chini ya kocha mkuu Musa Benjamin kwa motisha ambayo wamepata kambini tangu waanze maandalizi yao mwaka jana.

Okoth ambaye ni mshindi wa medali ya shaba katika mashindano ya kimataifa ya Konstantin Korotkov Memorial Cup nchini Urusi mwezi Mei, ameahidi kutia kibindoni medali katika mashindano haya ya Olimpiki anayoshiriki kwa mara ya pili.

Mabondia wengine, Elly Ajowi katika uzani wa heavy, Christine Ongare (fly) na Elizabeth Akinyi (welter) wana wingi wa imani kurudi nyumbani na ushindi baada ya maandalizi kabambe waliyopata kufikia sasa.

Aidha, bondia wa zamani wa timu ya taifa Ibrahim ‘Surf’ Bilali ambaye ni kati ya wakufunzi wa timu ya taifa walio kambini, amekisifu kikosi cha ‘Hit Squad’ akisema kiko imara.

Kwa mujibu wa naibu kocha David Munuhe, kikosi cha ‘Hit Squad’ kinatarajiwa kuondoka nchini Julai 18 kuelekea Tokyo, Japan kwa michezo ya Olimpiki.

You can share this post!

Brazil wakomoa Chile na kuingia nusu-fainali za Copa America

Kaunti zahimizwa kukumbatia mpango wa kufikisha ushauri wa...