Uingereza kigezoni wakijiandaa kuvaana na Ukraine kwenye robo-fainali za Euro

Na MASHIRIKA

UINGEREZA watajaribu leo kufuzu kwa nusu-fainali za Euro kwa upande wa wanaume kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25 watakaposhuka dimbani kuvaana na Ukraine leo usiku jijini Roma, Italia.

Baada ya kusubiri kwa miaka 55 kuangusha Ujerumani kwenye hatua ya mwondoano ya kipute hicho mnamo Juni 29, 2021 ugani Wembley, Uingereza watakutana na Jamhuri ya Czech au Denmark jijini London iwapo watashinda Ukraine.

Baada ya kusakata mechi zao nne za kwanza ugani Wembley, mchuano wa leo usiku utakuwa wa kwanza kwa Uingereza kusakata ugenini tangu kipute cha Euro king’oe nanga mnamo Julai 13, 2021.

Kwa sababu ya ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini Uingereza, mashabiki wa taifa hilo wameonywa dhidi ya kusafiri Italia. Hivyo, kuna uwezekano kwamba uwanja wa Olimpico jijini Roma utakuwa na idadi kubwa ya mashabiki wa Ukraine.

Southgate aliwaongoza Uingereza kutinga nusu-fainali za Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi.

Amesema wanasoka wake hawatakuwa na presha wakichezea ugenini tofauti na jinsi hali imekuwa katika michuano minne ya awali ugani Wembley.

Iwapo Uingereza watashinda Ukraine, basi watafuzu kwa nusu-fainali za Euro kwa mara ya kwanza tangu 1996.

Kufikia sasa, Uingereza hawajashindwa katika kipute cha Euro mwaka huu na hawajaokota bao lolote wavuni mwao.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO