• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
Ruto akausha mahasla

Ruto akausha mahasla

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amelaumiwa kwa kutoa zabuni ya ununuzi wa fulana na kofia zinazotumika katika kampeni jwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Kiambaa kwa wafanyabiashara wa Dubai badala ya wale wa humu nchini.

Hii ni kinyume na ahadi ya vuguvugu lake la The Hustler Nation la kuwapiga jeki wafanyabiashara wadogowadogo mfumo wa uchumi unaokuzwa kuanzia mashinani.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UDA, Veronica Maina jana alipuuzilia mbali madai hayo akisema bidhaa hizo za kampeni zilinunuliwa na kupigwa chapa humu nchini.

‘Ripoti hizo ni za uwongo. Fulana na kofia hizo zimepigwa chapa humu nchini,’ akaambia Taifa Leo kupitia ujumbe mfupi.

Lakini, Bi Maina hakufafanua kama zabuni hiyo ilipewa wafanyabiashara wadogo au mabwanyenye kulingana na falsafa inayovumishwa na UDA.

Suala hilo liliibuliwa na mwanablogu Wahome Thuku aliyedai kuwa ni kinaya kwa UDA kutoa zabuni ya ununuzi na kupiga chapa fulana na kofia kule Dubai huku ‘kazi ya ‘mama-mboga na mtu wa mkokoteni’ ikiwa ni kuvaa na kupigwa picha zao kuwekwa kwa Facebook, Twitter na YouTube.’

‘Hakuna hasla aliyepewa kazi ya kupiga chapa fulana (T-Shirts) na Caps (kofia) milioni 15 za kampeni. Ni ajabu kwamba mamilioni ya pesa za kazi hii yaliwaendea matajiri huku masikini wakiendelea kutengwa,’ akaandika Bw Thuku ambaye pia ni wakili.

Kauli hiyo ilichochea gumzo kali kwenye mtandao huo wa facebook kati ya wafuasi wa Dkt Ruto na wale walionekana kuwa mahasidi wake kisiasa.

‘Hii kauli-mbiu ya hasla ni njama fiche ya kuwadanganya maskini ilhali wao ni matajiri wa kupindukia. Sasa ona wanapeana tenda ya mamilioni huko Dubai huku mahasla halisi wakisahaulika,’ akasema Danstan Bwoma kwenye Facebook.

Kwa upande wake Leon Korir alisema: ‘Wahome Thuku akome kusambaza uwongo!. Tenda hii ilipewa Wakenya lakini wakaamua kuchapisha fulana hizo nje ya nchi.’

Mjadala huo pia ulimvutia Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro, aliyepuuzilia mbali madai ya Thuku akimtaja kama ‘mkereketwa wa Jubilee’ aliyekodiwa kuchafua sifa za vuguvugu la ‘The Hustler Nation’’.

Hata hivyo, tofauti na kauli ya Bi Maina, Bw Osoro alikiri kuwa bidhaa hizo ziliagizwa na kupigwa chapa Dubai.

‘Hasla Mkenya kutoka River Road alipewa tenda ya kuwasilisha kofia na fulana milioni 15 zilizopigwa chapa kwa bei ya humu nchini. Lakini kutokana na uhaba wa mashine uliosababishwa na ushuru wa juu uliowekwa na Uhuru, aliamua kupeana kazi hiyo nje,’ akasema Mbunge huyo ambaye ni mmoja wa wandani wa karibu wa Dkt Ruto.

‘Sasa Mwangi anatabasamu huku akisoma propaganda za Wahome Thuku ambazo hazitadumu. Hehehe…..’ Bw Osoro akaongeza.

Katika kampeni zake za kujinadi kama kiongozi anayefaa kuwa Rais wa tano nchini mwaka ujao, Dkt Ruto ameahidi kukumbatia mfumo wa uchumi unaokuzwa kuanzia tabaka la chini, ambalo ndilo lenye watu wengi, kuelekea juu.

Kulingana na naibu huyo wa rais, ambaye ametangaza kuwa atawania urais kwa tiketi ya chama cha UDA, wafanyabiashara wadogo ndio watakaofaidi chini ya utawala wake.

‘Katika serikali ambayo tutaunda mwaka ujao, Mungu akipenda, tutamuinua mama mboga, mtu wa boda boda, mtu wa mkokoteni na wale wengine wa kiwango hicho. Ustawi wetu wa kiuchumi utaanza kule chini,’ Dkt Ruto akasema juzi baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili mtaa wa Umoja, Nairobi.

You can share this post!

Wito EACC ichunguze maafisa wa elimu

Lusaka akiri kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na...