• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Aibu wizara muhimu zikiburuta mkia katika ripoti ya utendakazi

Aibu wizara muhimu zikiburuta mkia katika ripoti ya utendakazi

NA NDUNGI MAINGI

IMEKUWA fedheha kwa wizara zilizorodheshwa mkiani katika utendakazi kwenye ripoti ya 2019/2020 kwani ni zile zinazotegemewa  zaidi na wananchi. 

Wizara za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi; Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Ubunifu na Vijana; Michezo na Utamaduni na Utalii na Wanyama pori ziliburuta mkia katika ripoti hiyo.

Kwanza, wizara iliyoshika mkia ya Kilimo inaangazia sekta ambayo asilimia kubwa ya Wakenya wanategemea kukimu mahitaji yao ya kila siku.

Mapato kutokana na kilimo na ufugaji huchangia takriban asilimia 30 ya mapato ya kitaifa kupitia kwa mazao ya shambani na bidhaa tofauti zinazotokana na wanyama wa kufuga.

Hivyo basi, wizara hii inafaa kuwa kipaumbele katika kutimiza malengo yake ili kuwafaa Wakenya wengi wanaotegemea sekta hiyo.

Mawasiliano na Teknolojia, kwa upande mwingine, ni uti wa mgongo kaatika maisha ya sasa ambapo mbinu za mawasiliano na teknolojia zinazidi kuimarika.

Wizara hii ina jukumu kubwa katika jamii ya sasa, ikibainika kuwa mafunzo haya yatahusishwa katika mtaala mpya wa elimu(CBC), ambapo pia ubunifu utahusishwa.

Wizara za Michezo na Utamaduni, na Utalii na Wanyamapori zilipata pigo kutokana na mlipuko wa virusi vya corona. Shughuli nyingi za wizara hizo ziliathirika, lakini mawaziri wana majukumu ya kuziboresha.

Wizara ya Michezo na Utamaduni ina jukumu kubwa la kutimiza kwa nchi. Ni sekta ambayo inashabikiwa sana kupitia kwa michezo tofauti.

Nchi ya Kenya inajulikana kufana katika michezo tofauti ikiwemo riadha, voliboli, ragbi na michezo mingine.

Hivi karibuni, wachezaji wa voliboli ya ufukweni walifana huko Morocco, wanaume kwa wanawake. Wanariadha wametua Tokyo huku wachezaji wa vikapu wakipiga kambi nchini Rwanda.

Hii ina maana kuwa wizara hii inatarajiwa kujitolea kikamilifu kuboresha sekta ya michezo na kutimiza maazimio yake.

Kwa upande wa Utalii, ni wizara ambayo inaleta kipato kwa taifa. Mfano ni Mashindano ya Mbio za Magari ambayo yalileta kipato kwa taifa.

Wizara hii inafaa kuboreshwa wakati taifa linapojengwa upya kutokana na pigo la corona ili kuimarisha mapato ya nchi.

You can share this post!

Argentina wakung’uta Brazil na kutwaa taji la Copa...

Wawili wafariki mamia wakikesha nje baada ya nyumba...