• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:55 AM
Argentina wakung’uta Brazil na kutwaa taji la Copa America

Argentina wakung’uta Brazil na kutwaa taji la Copa America

Na MASHIRIKA

SUBIRA ya Lionel Messi kutia kapuni taji la kwanza katika soka ya kimataifa hatimaye ilimvutia heri Jumamosi usiku Argentina walipowakomoa wenyeji Brazil 1-0 na kunyanyua Kombe la Copa America.

Mechi hiyo iliyochezewa katika uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro, ilihudhuriwa na mashabiki 7,000 pekee kutokana na ukali wa kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona chini Brazil.

Baada ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa, Messi, 34, alijitupa chini kwa furaha. Nyota huyo ambaye sasa hana klabu tangu mkataba wake na Barcelona utamatike rasmi mnamo Juni 30, baadaye alibebwa juu kwa juu na wenzake wa Argentina.

Makala ya 47 ya Copa America mwaka huu ni kipute cha 10 cha haiba kubwa kushuhudia Messi akiwakilisha Argentina kimataifa. Chini ya unahodha wake, Argentina walikomesha ukame wa miaka 28 tangu wajizolee taji la Copa America kwa mara ya kwanza mnamo 1993 baada ya kupepeta Mexico 2-1 jijini Guayaquil, Ecuador.

Mabao manne yaliyofungwa na Messi kwenye kampeni za Copa America mwaka huu yalimvunia taji la Mchezaji Bora wa kipute hicho ambacho awali kilikuwa kiandaliwe kwa pamoja na Argentina na Colombia kabla ya kuhamishiwa Brazil.

Fowadi matata wa Paris Saint-Germain (PSG), Angel di Maria ndiye alifungia Argentina bao la pekee na la ushindi dhidi ya Brazil. Goli hilo lilichangiwa na Rodrigo de Paul anayechezea Udinese ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Brazil waliokuwa mabingwa watetezi walikosa kutamba katika ardhi yao ya nyumbani. Licha ya kumiliki asilimia kubwa ya mpira, wafalme hao mara tano wa dunia walipata fursa mbili pekee za kutatiza ngome ya Argentina. Hata hivyo, kipa Emiliano Martinez wa Aston Villa alidhibiti vilivyo makombora hayo aliyoelekezewa na Richarlson Andrade na Gabriel Barbosa.

Mfumaji tegemeo kambini mwa Brazil, Neymar Jr aliyewahi kucheza pamoja na Messi kambini mwa Barcelona kati ya 2013 na 2017, alijiinamia kwa masikitiko mwishoni mwa mechi kabla ya kupiga magoti na kuruhusu machozi kumtiririka kuwili.

Jeraha lilimnyima nyota huyo wa PSG fursa ya kunogesha fainali ya awali ya Copa America iliyoshuhudia Brazil wakizamisha Peru 3-1 mnamo Julai 8, 2019.

Miaka 15 imepita tangu Messi awakilishe Argentina kwa mara ya kwanza katika kipute cha haiba kubwa. Ushindi dhidi ya Brazil ni kitulizo kikubwa kwa sogora huyo ambaye sasa amechezea timu yake ya taifa mara 53 kwenye michuano ya fainali nne za Kombe la Dunia na sita za Copa America.

Messi alikuwa na presha ya kuzolea Argentina ufanisi huo ikizingatiwa kwamba ubabe unaomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji bora duniani ulikuwa ukidhihirika zaidi akisakata soka katika ngazi ya klabu.

Fowadi huyo anayehemewa pakubwa na PSG pamoja na Manchester City, amenyanyua mataji 10 ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na sita ya Ballon d’Or akivalia jezi za Barcelona.

Baada ya kufeli katika majaribio kadhaa ya kuvunia Argentina taji la kimataifa, Messi aliwahi kutangaza kustaafu – maamuzi aliyoyabatilisha – baada ya Argentina kupoteza fainali ya pili mfululizo ya Copa America mnamo 2016.

Fainali ya 2016 ilikuwa ya tatu kwa Messi kupoteza kwenye Copa America na walichapwa na Chile 4-2 miaka miwili pekee baada ya Ujerumani kuwazamisha 1-0 kwenye fainali ya Kombe la Dunia.

Messi anatarajiwa pia kuongoza Argentina katika fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa nchini Qatar mnamo 2022. Kipute hicho kitampa supastaa huyo fursa ya mwisho ya kujaribu kushinda taji hilo ambalo Argentina hawajawahi kunyanyua tangu 1986.

Argentina walishuka ulingoni kuvaana na Brazil wakilenga  kuendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mchuano wowote tangu 2019.

Kikosi hicho kimekuwa kikijivunia mwamko mpya chini ya mkufunzi Lionel Scaloni tangu kibanduliwe mapema na Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi. Mikoba ya Argentina ilikuwa ikidhibitiwa na kocha Jorge Sampaoli wakati huo.

Baada ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Chile katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi A, Argentina walishinda mechi tatu walizosalia nazo na kukamilisha kampeni za kundi lao kileleni. Walipepeta Bolivia 4-1 baada ya kusajili matokeo ya 1-0 dhidi ya Uruguay na Paraguay.

Ushindi wa 3-0 waliosajili dhidi ya Ecuador kwenye robo-fainali uliwapa motisha ya kudengua Colombia kwa mabao 3-2 kupitia penalti baada ya kuambulia sare ya 1-1 kufikia mwisho wa muda wa kawaida.

Kwa upande wao, Brazil ambao ni mabingwa mara tisa wa Copa America, walifungua kampeni za mwaka huu kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Venezuela mnamo Juni 14. Walilazimishiwa sare ya 1-1 na Ecuador baada ya kucharaza Peru 4-0 na Colombia 2-1 katika mechi nyinginezo za Kundi B. Walipepeta Chile 1-0 kwenye robo-fainali kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Peru kwenye nusu-fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Maangi asema atahepa Ruto Matiang’i akiwania

Aibu wizara muhimu zikiburuta mkia katika ripoti ya...