• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
MUTUA: Mbona hasira za Wakenya zinaishia kuuana kiafriti?

MUTUA: Mbona hasira za Wakenya zinaishia kuuana kiafriti?

Na DOUGLAS MUTUA

HIVI sisi tunaowapenda watoto kwa jumla tutawadekeza na kuwaburudisha vipi bila kusingiziwa nia ya kuwateka na kuwang’oa macho na jamii hii yenye chuki na hasira?

Wajomba tutawatembeza na kuwanunulia zawadi wapwa wetu vipi kama tulivyozoea bila kusingiziwa kuwateka kisha tuishie kupigwa kwa mawe na kukatakatwa kwa mapanga?

Mimi baba nitaanza kutegemea hisani ya wanangu wachanga kuniokoa kwa kunitambulisha hadharani iwapo nitatembea madukani nao kisha nishukiwe kuwateka?

Wafanyabiashara nao watatafutaje viwanja na mashamba ya kununua iwapo hawawezi kutembezwa vinakouzwa kwa kuwa watasingiziwa nia ya utekaji na kuuawa kinyama?

Kenya inaelekea kuwa nchi ya wendawazimu na wapumbavu wanaotafakari baada ya kufanya maovu ya kukata maini kama kupiga watu kitutu na kuwaua.

Kisa ambapo mfugaji wa ng’ombe wa maziwa eneo la Kilifi, dereva wake na wakala wa ardhi waliuawa kwa kushukiwa kuwa watekaji kinasikitisha na kuhofisha si haba.

Mfugaji Sidik Anwarali Sumra, dereva wake kwa jina Rahil Mohamed Kasmani na wakala wa ardhi, Bw James Kazungu Kafani, waliangamizwa kinyama wiki jana kijijini Junju, Kilifi.

Walivamiwa kwa mapanga na silaha nyingine duni, wakateswa vibaya mno hadi wakafariki, kisha miili yao ikakokotwa kwa bodaboda. Huo ni uhayawani hasa!

Watatu hao walivamiwa walipokuwa wakizuru ardhi fulani kijijini humo, ziara iliyoongozwa na Bw Kafani. Bw Sumra alinuia kununua ardhi inayodaiwa kukaliwa na maskwota.

Kisa hicho kinanikumbusha kingine kilichotokea mtaani Zimmerman, Nairobi, mwezi Juni, ambapo wananchi waliwavamia watu waliosafiri na mtoto asiyekuwa wao.

Hao walikuwa na bahati kama mtende kwa kuwa walinusurika kifo, lakini tayari walipata kipigo kibaya na gari lao likavunjwavunjwa vioo kwa mawe.

Kwani maisha ya binadamu yamekosa thamani kiasi gani hivi kwamba mshukiwa anavamiwa au kuuawa kiholela kabla ya tuhuma dhidi yake kuthibitishwa?

Huo ni ushamba, kichaa au watu wanatafuta visingizio vya kujiondolea hasira ambazo zinatokotea ndani kwa ndani kama volkeno na hivyo hazina budi kujilipukia ovyo?

Tukizingatia kisa cha Bw Sumra na wenzake kwa mfano, tunakubaliana kwamba ardhi ni suala nyeti kote nchini. Migogoro ya umiliki wa ardhi ikianzia jijini inaishia kijijini.

Si nadra kwa tajiri yeyote kufika eneo linalozozaniwa, akiongozwa na wakala, na kudai hiyo ni ardhi yake na hivyo basi wanaoikalia wanapaswa kuhama.

Si mara ya kwanza kwa watu – maskwota au hata watu wanaomiliki ardhi zao kihalali – kuamka asubuhi na kupata ilani milangoni wakitakiwa kuhama lau sivyo wafurushwe.

Watu wa Pwani, ambao kwa kweli wamekumbwa na matatizo ya ardhi zaidi ya wakazi wa maeneo mengine tangu Kenya iwe huru, hawana pupa ya kupiga wala kuua.

Karibu wakati wote wao hushtaki kwa wakuu wa serikali au hukimbia mahakamani ikiwa wana uwezo, kuvamia na kuua haiwi hatua ya kwanza kabisa.

Bw Sumra hata hakuwa amenunua ardhi hiyo, alikuwa amekwenda kuiona tu ili aamue iwapo angeinunua kisha ahamishie mradi wake wa ufugaji hapo.

Mradi huo ambao umenawiri kwa miaka mingi tu ungeleta maendeleo na fursa za kazi kwa wenyeji.

Na kwa sababu alikuwa mwenyeji wa Pwani, labda hangenunua ardhi hiyo iwapo ubishi ungezuka kuihusu kwani kufanya hivyo kungeuhatarisha.

Sijui iwapo chanzo cha hasira za wananchi ni matatizo ya kiuchumi yaliyozidishwa na janga la korona na serikali isiyowajali, lakini kuna jambo.

Na linapaswa kuchunguzwa na kutafutiwa suluhu kabla ya Kenya kulipuka kama Afrika Kusini, taifa ambapo watu husubiri kisingizio cha kuharibu na kupora mali.

Maskini watakapokosa chakula kabisa, chaguo la pekee litakuwa kuwala matajiri. Hakuna atakayekuwa salama, hivyo ni heri tudhibiti hali mapema tusiishie kulana kinyama.

You can share this post!

KAMAU: IEBC ijenge imani ya uwajibikaji miongoni mwa Wakenya

Waziri apongeza Lionesses kujikatia tiketi ya fainali ya...