Vipusa wa Zambia wapondwa 10-3 na Uholanzi kwenye Olimpiki

Na MASHIRIKA

TIMU ya taifa ya Zambia ambayo inashikilia nafasi ya 104 kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), ilipondwa na Uholanzi 10-3 kwenye ufunguzi wa soka ya Olimpiki miongoni mwa wanawake.

Fowadi wa Arsenal, Vivianne Miedema alifungia Uholanzi ambao ni miamba wa bara Ulaya jumla ya mabao manne huku aliyekuwa mwenzake kambini mwa Arsenal, Danielle van de Donk akicheka na nyavu mara tatu.

Nahodha wa Zambia, Barbra Banda pia alifunga mabao matatu licha ya kikosi chake kubebeshwa gunia la magoli.

Kwingineko, fowadi Marta alifunga mabao mawili na kusaidia Brazil kupepeta China 5-0.

Nyota huyo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kufunga katika jumla ya mechi tano mfululizo kwenye Olimpiki. Kwa sasa anajivunia mabao 12.

Kwa upande wake, beki Formiga, 43, aliendeleza rekodi ya kunogesha Olimpiki saba mfululizo tangu soka ya wanawake ianzishwe kwenye mashindano hayo mnamo 1996.

Uingereza walianza vyema kampeni zao za Olimpiki kwa kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Chile kwenye Kundi E. Walifungiwa mabao yao na Ellen White.

Katika mechi nyingine ya Kundi E, wenyeji Japan waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Canada baada ya kiungo wa Arsenal, Mana Iwabuchi wa Japan kufuta juhudi za Christine Sinclair aliyewaweka Canada uongozini mwanzoni mwa kipindi cha kwanza. Kipa Stephanie Labbe wa Canada pia alipangua penalti kwenye gozi hilo.

Sinclair aliendeleza rekodi ya mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Canada. Sasa anajivunia mabao 187 na ndiye mchezaji wa nne katika historia kuwa kuchezea taifa lake jumla ya mechi 300.

Katika mchuano mwingine wa Jumatano, Australia walikomoa New Zealand 2-1 baada ya fowadi wa Chelsea, Sam Kerr kufunga bao na kuchangia jingine.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

ReplyForward