• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:10 PM
Uchaguzi: EACC yataka watumishi wajiuzulu kwanza

Uchaguzi: EACC yataka watumishi wajiuzulu kwanza

FARHIYA HUSSEIN na VALENTINE OBARA

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imewataka watumishi wa umma ambao wanaendeleza kampeni wakipanga kuwania nyadhifa za kisiasa mwaka 2022, wajiuzulu mara moja.

Viongozi wa kisiasa wanazidi kuendeleza kampeni za mapema kinyume cha sheria, huku ikiwa imesalia takriban mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Miongoni mwa walioanza kujipigia debe mapema kwa siasa za 2022 ni wanaopanga kuwania kiti cha urais, ugavana, useneta, ubunge na udiwani.

Hii ni licha ya kuwa, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), iliratibisha kampeni za uchaguzi zianze rasmi Mei 30, 2022 hadi Agosti 6, 2022.

Baadhi ya watumishi wa umma wakiwemo mawaziri na makatibu wa wizara pia wameonekana wakijipigia debe wanapojiandaa kuwania viti vya kisiasa mwaka ujao.

Kulingana na ratiba ya maandalizi ya uchaguzi iliyotolewa na IEBC, watumishi wa umma watahitajika wawe wamejiuzulu ifikapo Februari 9, 2022 ikiwa wanataka kuwania viti vya kisiasa.

“Kuna maafisa wa utumishi wa umma ambao tayari wamejitosa katika kampeni kali za kisiasa huku wakiegemea pande tofauti za vyama vya kisiasa. EACC inahitaji mtumishi yeyote wa umma anayetamani kuingia siasa kwa maandalizi ya 2022 ajiuzulu, au wawe na subira hadi wakati ufaao utakapofika,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Twalib Mbarak.

Akizungumza jjini Mombasa wakati wa kongamano la wadau wa kupambana na ufisadi, Bw Mbarak alisema mienendo ya watumishi wa umma kupiga kampeni wakati bado wako afisini ni ukiukaji wa sheria za maadili mema.

Wiki iliyopita, baadhi ya wanasiasa walitaka IEBC ichukue hatua za haraka dhidi ya wanasiasa ambao tayari wanaendeleza kampeni zao za 2022.

Seneta wa Kaunti ya Kilifi, Bw Stewart Madzayo, alilalamika kuwa kuna wanasiasa ambao tayari wameanza kusambaza mabango na fulana zinazoeleza maazimio yao ya kisiasa ya 2022.

Alimtaka Mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanasiasa husika.

“IEBC pekee ndiyo inastahili kusimamia kampeni zote zinazofaa kufanywa nchini. Hakuna wakati Chebukati amesema uchaguzi utafanywa siku 90 zijazo ndipo watu waanze kuchapisha mabango na fulana za kampeni. Yale yanayofanyika Kilifi ambapo watu wanazunguka na mabango ni hatia. Chebukati anafaa achukue hatua,” akasema Bw Madzayo.

Katika hafla ya jana, Bw Mbarak alisema faili 85 za madai ya ufisadi zimepelekwa kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na upelelezi unaendelezwa.

Pia alisema kufikia sasa ardhi zinazogharimu Sh17.8 bilioni na Sh38.4 bilioni zimerudishwa.

You can share this post!

Pendekezo vyeti vya kuzaliwa vitumike kusajili wapigakura

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa Kiambu washauriwa...