• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
TAHARIRI: Tuchague viongozi kwa msingi wa sera

TAHARIRI: Tuchague viongozi kwa msingi wa sera

KITENGO CHA UHARIRI

INASIKITISHA kwamba Kenya na mataifa mengine mengi ya bara Afrika yana mazoea ya kuwachagua viongozi wao wa kisiasa kwa msingi wa kikabila.

Hii ni tofauti na nchi za Magharibi kama vile Uingereza na Amerika ambazo raia wazo huwachagua viongozi wao kwa msingi wa sera, sifa na falsafa bali si kabila au hata rangi.

Hii ndiyo maana utampata kiongozi maarufu nchini Amerika, aliye katika nafasi nzuri ya kushinda ama urais, useneta, ugavana au ubunge, anakataliwa na wapiga-kura katika dakika ya mwisho pindi panapoibuka kashfa yoyote kumhusu.

Yaani raia wa nchi hii humuepuka mtu yeyote mwenye sifa mbaya kuchaguliwa katika wadhifa wowote. Lakini hali ni kinyume nchini humu ambapo baadhi ya makabila yamekuwa yakiwachagua viongozi wenye sifa au mienendo ya kutiliwa shaka eti kwa sababu ni mtu wao.

Hii hasa hufanyika hivi iwapo kashfa ya mhusika huyo imeibuliwa na mwanasiasa kutoka kabila tofauti, kwa hivyo kiongozi huyo mwenye kashfa huchaguliwa kama njia ya kumwadhibu yule mwanasiasa ‘hasimu’ kutoka kabila tofauti

Tunapoelekea katika uchaguzi ujao wa mwaka 2022, kuna hatari ya taifa hili kurudia kosa hilo la kuwachagua viongozi wake kutokana na nasaba, kabila au kutumia vigezo vinginevyo ambavyo hakika havifai kuzingatiwa.

Kwa sababu hiyo, ombi letu ni kuwa katika uchaguzi ujao, kabila lisiwe kigezo cha kutumiwa hata kidogo.

Ukabila huu ndio hutufumba macho kuwateua viongozi wadhaifu kisha baada ya muda mfupi, makosa yao yakaanza kuchipuka nasi tukawa tumechelewa; chambilecho wahenga maji yakimwagika hayazoleki.

Aidha, maadamu ustawi wa nchi huenda sako kwa bako na hadhi ya viongozi wanaochaguliwa, iwapo twaitakia nchi yetu, kaunti au eneobunge letu mafanikio, sharti tubadilishe kigezo tunachotumia.

Pia ifahamike kuwa wapo baadhi ya viongozi ‘matapeli wa kisiasa’ ambao wataibuka na sera nzuri hasa kupitia manifesto zao wakati wa kampeni lakini unapozichunguza kwa jicho la ndani, unagundua kuwa ni hadaa tupu kwa sababu hazitekelezeki.

Hii ina maana kuwa sharti maelezo ya kina yatolewe na mwanasiasa mhusika kuhusu jinsi atakavyotekeleza sera zake.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Wakazi Limuru katika njiapanda kuhusu...

KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa wajiepushe na mjadala...