• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Bei ya chai sasa yapanda kanuni mpya zikianza kuzaa matunda

Bei ya chai sasa yapanda kanuni mpya zikianza kuzaa matunda

Na ANITA CHEPKOECH

MAUZO ya chai katika mnada wa Mombasa yameimarika hadi kiwango cha asilimia 87, baada ya kudorora kwa muda mrefu.

Imariko hilo linatokana na kanuni zilizowekwa na Shirika la Ustawi wa Sekta ya Majani Chai Nchini (KTDA).

Shirika hilo lilisema uamuzi wake wa kuanzisha mpango wa bei ya wastani ambayo chai inapaswa kuuzwa, ulilenga kuhakikisha kuwa wakulima wanapata faida, na umeanza kuzaa matunda.

Katika taarifa, KTDA ilisema kuwa viwanda vinavyofungamana nayo, viliuza asilimia 87 ya majani chai yaliyowasilishwa katika mnada wa chai mnamo Julai 27. Hii ni kutokana na mauzo ya kiwango cha asilimia 19 katika wiki iliyotangulia.

“Chai iliuzwa kwa bei wastani ya Sh248 kwa kilo moja ikilinganishwa na Sh217 kwa kilo katika mnada wa mwaka jana na Sh206 kwa kilo wiki tatu zilizopita. Hii ni kabla ya kuwekwa kwa bei ya chini kabisa ambayo chai inafaa kuuzwa,” KTDA ikasema.

Bodi mpya ya KTDA iliweka bei ya Sh263 kwa kilo moja ya chai iliyotayarishwa mnamo Julai 10. Hatua hiyo imechangia kupungua kwa ununuzi wa chai katika mnada huo ili kutoa nafasi kwa soko kujifahamisha na mwongozo huo mpya.

Ufanisi huo ni baraka kwa zaidi ya wakulima 600,000 wanaohudumiwa na KTDA na ambao kwa muda mrefu wameathirika kutokana na bei duni.

“Tumefurahishwa na kuimarika kwa mauzo ya chai katika mnada, na hii inaashiria kuwa wanunuzi wetu wanatambua haja ya kustawishwa kwa kilimo cha majani chai,” akasema Bw Wilson Muthaura, kaimu mwenyekiti wa KTDA. Bei ya chai katika mnada wa Mombasa imekuwa ikishuka tangu 2018 na mwaka huu ikashuka hadi Sh200. Hali hii ilitishia kuwasababishia wakulima hasara.

Mbali na suala la bei, bodi ya KTDA pia imevitaka viwanda vya majani chai kupunguza gharama ya utayarishaji kilo moja ya chai huku wakilenga kuimarisha ubora wa zao hilo ili kuvutia bei bora.

You can share this post!

Ruto hatimaye afafanua mfumo wa ‘Bottom-up’

Dressel aweka rekodi mpya kwenye uogeleaji wa 100m butterfly