• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:03 AM
Wanafunzi wanaougua corona hawaonyeshi dalili – Kagwe

Wanafunzi wanaougua corona hawaonyeshi dalili – Kagwe

Na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe ameonya kuwa endapo wananchi hawatachukua tahadhari na kujikinga kutokana na virusi vya corona huenda taifa likajipata katika hatari ya kushindwa kudhibiti msambao.

Bw Kagwe amesema maambukizi ya Covid-19 yanayoendelea kushuhudiwa, msambao unaendelezwa na wanafunzi.

Alisema wanafunzi wengi walioambukizwa hawaonyeshi dalili, suala alilotahadharisha ikiwa watu hawatatilia maanani sheria na mikakati iliyowekwa watajipata katika hatari.

“Idadi kubwa ya wanafunzi waliothibitishwa kuambukizwa Covid-19 hawaonyeshi dalili. Wanapoenda nyumbani wanasambazia wazazi na wanaoishi nao.

Nao wanapoenda maeneo yao ya kazi wanaambukiza wenzao. Hivyo ndivyo virusi vinaenea, na ni hatari,” Bw Kagwe akasema.

Waziri amewataka walimu wote kuhakikisha wamepata chanjo ya corona, ikizingatiwa kuwa wao ndio wako katika hatari zaidi ya kuambukizwa.

“Ifahamike kuwa hakuna upungufu wa chanjo ya walimu. Wahakikishe wamepata chanjo,” akahimiza.

Visa vya maambukizi ya corona vimeendelea kuongezeka, hasa baada ya shule kufunguliwa na wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza kuanza kusajiliwa juma hili kwenye shule walizoitwa.

Kenya imeingia katika mkumbo wa nne wa maambukizi ya Covid-19, virusi hatari aina ya Delta Variant kutoka India vikiendelea kusambaa.

Wizara ya Afya tayari imekiri baadhi ya hospitali kujaa wagonjwa, kiasi cha vitanda vya kuwalaza kupungua.

You can share this post!

Nitagura Jubilee kwa hiari ila si kwa kushurutishwa –...

Wahitimu 6,500 kutoka MKU washauriwa wawe wabunifu