• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Raila azuru TZ akiwa njiani kurejea Kenya kutoka Zambia

Raila azuru TZ akiwa njiani kurejea Kenya kutoka Zambia

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga, Jumatano alifanya ziara ya siku moja nchini Tanzania, akiwa njiani kurejea nchini kutoka Zambia ambako alikuwa ameungana na viongozi kadha wa Afrika kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Zambia Hakainde Hichilema.

Bw Odinga alikutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Dar es Salam kwa mashauriano.

Kwenye ujumbe kupitia akaunti yake ya Twitter, waziri huyo mkuu wa zamani alisema kuwa mazungumzo kati yake na Rais Suluhu yalihusu namna ya kuimarisha ujenzi wa miundomsingi katika eneo zima la Afrika Mashariki.

“Vile vile, tulijadili njia mbalimbali za kuimarisha uchukuzi wa majini katika ukanda wa Afrika Mashariki kupitia Ziwa Victoria,” Bw Odinga akasema.

Baadaye kiongozi huyo, ambaye ni Mjumbe Mkuu wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu miundomsingi, aliwatembelea wajane wa waliokuwa marais wa Tanzania, Benjamin Mkapa na John Pombe Magufuli.

“Nilipitia kutembelea familia za marafiki zangu wa dhati Marais Benjamin Mkapa na John Magufuli. Ilikuwa furaha yangu kumwona Mama Mkapa na Mama Janeth Magufuli wakiwa wachangamfu. Mungu azilaze roho zao (marais hao wawili) mahali pema peponi,” Bw Odinga akasema kupitia ujumbe katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter.

Marehemu Mkapa aliyehudumu kama Rais wa tatu wa Tanzania alifariki mnamo Julai 24, 2020 ilhali marehemu Magufuli ambaye alihudumu kama Rais wa tano wa nchi hiyo alifariki mnamo Machi 17, 2021.

Bw Odinga aliandamana na bintiye Winnie Odinga katika ziara hiyo.

Rais Hichilema, ambaye amehudumu kama kiongozi wa upinzani kwa muda mrefu akiwania urais mara tano, aliapishwa rasmi mnamo Jumanne Agosti 24. Hii ni baada ya kupata ushindi mkubwa dhidi ya Rais anayeondoka Edgar Lungu katika uchaguzi mkuu uliofanyika juma moja lililopita ikiwa mara yake ya sita.

Bw Hichilema aliyeapishwa kama Rais wa saba wa Zambia alipata kura 2.8 milioni huku Bw Lungu akipata kura 1.8 milioni katika uchaguzi huo wa kihistoria.

Bw Odinga aliwasili nchini Zambia mnamo Jumatatu na kumtangulia Rais Uhuru Kenyatta aliyesafiri Jumanne asubuhi kwa ajili ya kuhudhuria hafla hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Kitaifa wa Mashujaa (National Heroes Stadium) jijini Lusaka, Zambia.

You can share this post!

Wakazi wa Thika wajitokeza kwa wingi kupata chanjo ya...

Kenya kusaka medali katika Olimpiki za Walemavu leo