• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MUTUA: Afrika yafaa ijitengenezee chanjo, iache kulalamika

MUTUA: Afrika yafaa ijitengenezee chanjo, iache kulalamika

Na DOUGLAS MUTUA

ALIWAHI kusema wakati mmoja Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kwamba hawaonei imani Waafrika wanaombukizwa ugonjwa wa corona na kuangamia.

Alihoji kwamba Mwafrika anaonyesha upumbavu wake anapokabiliwa na janga kisha kuketi kitako akisubiri kusaidiwa badala ya kufurukuta na kujitafutia suluhisho.

Wakati huo sikukubaliana naye, hasa kwa sababu alionekana kutojali hisia za waliofiwa na jamaa zao, lakini sasa ninamuelewa kwa kiasi fulani.

Ndiyo maana nadhani Rais Uhuru Kenyatta juzi ametoa kisingizio cha kuaibisha kuhusu uzembe wa mataifa ya Afrika katika kuwapa raia chanjo za kuzuia ugonjwa wa corona.

Uhuru alisema mataifa ya Afrika yalikuwa tayari kutoa chanjo zenyewe kuanzia mwanzo, lakini mataifa ya kizungu yakatumia ubaguzi wa rangi katika ugavi wa chanjo hizo.

Kwa maoni yake, ubaguzi wa rangi ulitokea kwa sababu mataifa tajiri yaliyotengeza chanjo yalizitumia kukinga raia wake kwanza badala ya kuuzia mataifa ya Afrika.

Alidai Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Afrika Kusini ziliweka mikakati kwa kuipa kandarasi kampuni fulani ya India ili kutoa chanjo zikipatikana.

Rejelea neno ‘zikipatikana’.

Hivi chanjo hizo zingepatikana kutoka wapi? Bila shaka uzunguni. Kwa hivyo Afrika nzima haikuwa na mpango wa kujitengezea chanjo? La.

Tatizo liko hapo: bara zima, lenye watu na akili zao waliosoma na kubobea kwenye fani ya sayansi kiasi cha kufanya kazi uzunguni, halikujaribu kuunda chanjo.

Lilisubiri mataifa yaliyoendelea yatengeze kisha yaligawie, hilo lilipokosa kutokea ikawa nongwa! Waafrika tutakoma kuonyesha hadharani udhaifu wetu wa kutegemea nundu.

Iwapo taifa la watu, kwa mfano Marekani, limewekeza katika utafiti na likapata chanjo, tuna haki gani kulalamika likiwajibika na kuwakinga watu wake na maradhi kwanza?

Halina jukumu lolote kisheria wala kibinadamu kuwafaa wazembe kwanza. Inabidi wazembe wasubiri kupewa masazo ya chanjo taifa la watu likitosheleza mahitaji yake.

Huku sisi tukiendelea kuzozania vyeo na kupora mali ya umma, sikwambii na michango ya kudhibiti corona, mataifa mengine yamekuwa mbioni kutafuta suluhu.

Na kwa sababu hilo ni janga la kimataifa, mataifa yaliyoendelea yanajua muhimu zaidi ni kuzuia maradhi husika yasienee ndani ya mipaka yake, si kufanya biashara ya dawa.

Kumbuka jukumu la kimsingi la mataifa hayo ni kuwakinga raia wanaolipa ushuru, si wengine wanaosubiri misaada au fursa za biashara.

Ni kwa sababu hiyo ambapo chanjo zinatolewa kwa raia wa Marekani, Uingereza, Ufaransa na mataifa mengineyo yaliyoendelea bila malipo yoyote.

Huo unaitwa ulinzi wa afya na ni sharti kwanza ufanyike kwenye mataifa yaliyojiundia chanjo kisha yaangaze macho kwingine.

Si kwamba yana jukumu la kufanya hivyo bali ni katika zile harakati za kujiweka salama kikamilifu ili wasiojikinga wasieneze aina nyingine za maradhi hayo hadi kwao.

Hata chanjo unazosikia zikitolewa kama misaada kwa Afrika ni katika kuufanikisha mkakati huo wa ulinzi wa afya, si kwamba Afrika inapendwa sana.

Wanasayansi wanasema kadiri maradhi yanayotokana na virusi yanavyokaa miongoni mwa watu ndivyo yanavyobadilikabadilika, hivyo inakuwa vigumu kuyaundia chanjo.

Na kwa sababu hawawezi kuunda chanjo mpya kila maradhi yanapobadilika, inakuwa dharura kuzuia maambukizi mapya kabisa kwa kuwapiga chanjo watu wote ikibidi.

Malalamiko ya Rais Kenyatta hayana mashiko kamwe bali yanaisawiri Afrika kama mkusanyiko wa watu wasiotumia akili kujikinga na hatari, wanaosubiri hisani ya watu.Tofauti hapa ni za kimtizamo.

Afrika inadhani mafedha – na mengi ni ya kukopa au kuchangisha – yanaiweka katika nafasi nzuri ya kupata chanjo.

Nayo mataifa yaliyoendelea yanajali zaidi afya ya raia, si faida ya mauzo ya chanjo, ndiyo maana yanazipa kampuni binafsi kandarasi za kutengeneza chanjo kwa mamilioni.

Itabidi viongozi wa Afrika wazinduke kutoka usingizi wa pono waliolala, wafadhili tafiti za kisayansi na kuwahimiza wanasayansi wetu wawe na uthubutu ili watuweke salama.

[email protected]

You can share this post!

Leicester City kupimana ubabe na Napoli katika Europa League

Msajili wa Vyama avunjilia mbali NASA