• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MKU yapokezwa cheti maalum kwa kutambulika kama kituo rasmi cha kutuza wahitimu vyeti halisi vya masomo

MKU yapokezwa cheti maalum kwa kutambulika kama kituo rasmi cha kutuza wahitimu vyeti halisi vya masomo

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) na kile cha Meru cha Sayansi na Teknolojia, vimetambulika kama vyuo vilivyo na vibali rasmi vya kutoa vyeti halisi vya masomo.

Kibali hicho kimetolewa rasmi na Mamlaka ya Kitaifa ya Kuainisha Kufuzu kwa Asasi za Elimu ya Juu – Kenya National Qualifications Authority (KNQA).

Mwenyekiti wake Dkt Kiremi Mwiria alisema vyuo hivyo viwili pia ni miongoni mwa vyuo vilivyojiandikisha kwa KNQA kwa mara ya kwanza.

Dkt Mwiria pia alithibitisha kuwa nayo Mamlaka ya Kitaifa ya Mafunzo ya Kiufundi, yaani National Industrial Training Authority ( NITA), imepewa mamlaka ya kushughulikia maswala ya kiufundi katika vyuo vya mafunzo.

Katika hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki, vyeti 728 vilitolewa na KNQA ambapo NITA ilipokea vyeti 416, MKU 198 huku nacho chuo kijulikanacho kama Bandari Academy kikipokea 92 na baadaye 22 mtawalia.

MKU ilipokea tuzo ya Qualification Awarding Institute mnamo Septemba 2020.

Dkt Mwiria alisema mpango huo una lengo la kuondoa vyeti ghushi katika elimu ya juu katika vyuo vya nchini Kenya.

Alisema mpango huo upo katika mipango yao maalum na mikakati ya miaka mitano kutoka mwaka jana 2020 hadi ifikapo mwaka 2025.

“Tunajaribu kuangazia mambo mengi ili kuondoa wale ambao wamezoea kughushi vyeti ili wapate kazi za kifahari. Tunataka kila mwanafunzi ale jasho lake kutoka kwa bidii masomoni,” alifafanua Dkt Mwiria.

Naibu Chansela wa MKU Prof Deogratius Jaganyi alisema maswala muhimu yapo katika maandishi kwenye kitabu cha ‘National Qualification Handbook’ kilichochapishwa mwaka wa 2018).

Pia alisema tayari chuo hicho kimeorodheshwa katika National Academic Impact SDG 10 Hub kati ya mwezi Juni 2021 na mwezi Mei 2024.

Alisema mipango hiyo yote inaendeshwa na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu yaani Commission for University Education programmes.

Waziri wa Leba Bw Simon Chelugui alisema huo ni mwelekeo ufaao. Alisema wale walio na ujuzi wa kazi ndio wana nafasi bora kupata ajira.

“Vyeti maalum vitakuwa muhimu kuleta mwelekeo bora katika soko la ajira,” alisema Bw Chelugui.

Naye Waziri Msaidizi (CAS) katika Wizara ya Elimu Noor Hassan alisema kuwa na eneo moja lililo na majina ya wale waliohitimu bila shaka kutapunguza ulaghai wa kutoa vyeti ghushi na “tutapata masomo yanayotambulika rasmi.”

You can share this post!

Tottenham wakomoa Watford na kudhibiti kilele cha jedwali...

Mwanachama wa Mungiki atisha kuua landilodi