• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Sheria njiani kupunguza walinzi wa DP hadi 30

Sheria njiani kupunguza walinzi wa DP hadi 30

Na IBRAHIM ORUKO

WIZARA ya Usalama wa ndani, inapendekeza maafisa wa usalama wa kumlinda naibu rais wasiwe zaidi ya 30. Haya yanajiri siku moja baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i kufichua kwamba, Naibu Rais William Ruto analindwa na maafisa 257.

Wizara hiyo inasema idadi ya walinzi wanaodumisha ulinzi kwa naibu rais inafaa kuthibitiwa ili kuepuka matumizi mabaya ambayo yamefanya baadhi ya maafisa wa umma kutengewa maafisa wengi kuliko wanaohitaji.

Maelezo kuhusu sheria hiyo iliyopendekezwa yalifichuliwa wakati wa kikao cha siri kati ya kamati ya bunge kuhusu usalama na waziri Matiang’i Jumatano.

Kamati inayosimamiwa na Mbunge wa Lari, Peter Mwanthi, ilifurahishwa na sheria hiyo mpya na ikaagiza wizara kuharakisha kuandaa mswada baada ya kuibuka kuwa naibu rais ana walinzi 257 wanaolinda makazi na biashara zake tofauti wakati ambao nchi inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama.

Wizara ilikuwa imeomba kamati kuandaa mswada lakini wabunge wakakataa ombi hilo wakisema wizara, ambayo inahusika na mahitaji ya usalama wa nchi inastahili kufanya hivyo.

“Kuna dharura ya kuwa na sheria hiyo na wizara iko katika hali nzuri kuitayarisha kwa kuwa ina maafisa wanaoelewa masuala hayo,” Bw Mwanthi aliambia Taifa Leo jana.

“Tunataka wizara kuandaa sheria hiyo kwa sababu ina makamanda wanaoelewa jinsi ya kukabili suala la usalama na ulinzi wa watu mashuhuri,” aliongeza.

“Suala hili ni la dharura. Tunataka mswada huo ndani ya wiki mbili au tatu. Wacha wautayarishe na kutuletea ili tuweze kuuchunguza na kuona tunachoweza kuongeza, kutoa au kuukubali ulivyo kwa sababu kinachotendeka kwa sasa hakiwezi kuruhusiwa kuendelea,” alisema Bw Mwanthi.

Pendekezo la kuwa na sheria kuhusu idadi ya walinzi wanaofaa kulinda watu mashuhuri liliibuka katika mawasilisho ya waziri kwa kamati alipokuwa akifafanua mabadiliko katika ulinzi wa Dkt Ruto ambayo yalizua mdahalo mkali.

Mbali na kuweka idadi ya walinzi wa naibu rais kuwa 30, wizara inapendekeza walinzi wa mawaziri na viongozi wa bunge- viongozi wa wengi na viranja- wasiwe zaidi ya wanne huku kila mbunge akiwa na mlinzi mmoja.

Hata hivyo wizara ilipendekeza mazungumzo kati ya mihimili mitatu ya serikali ili kufahamu mahitaji ya usalama ya Jaji Mkuu na maspika wawili wa bunge.

You can share this post!

Amani: Museveni aombwa atumie busara Sudan Kusini

Shule zakosa maji ya kupikia watoto