• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Madereva Wahome, Hamza na Kimathi kupeperusha bendera ya Safaricom mbio za Ramisi Rally

Madereva Wahome, Hamza na Kimathi kupeperusha bendera ya Safaricom mbio za Ramisi Rally

Na GEOFFREY ANENE

MAKINDA walio katika mradi wa kukuzwa na Shirikisho la Mbio za Magari Duniani (FIA Rally Star) Hamza Anwar, Mc Rae Kimathi na Jeremy Wahome wako tayari kuonyeshana kivumbi katika KCB Ramisi Rally mnamo Septemba 18.

Duru hiyo ya sita ya Mbio za Magari za Kitaifa za Kenya (KNRC) inafanyika katika kaunti ya Kwale.

“Matarajio yangu ni kuimarisha matokeo ya duru mbili zilizopita ambazo nilikamata nafasi ya tano. Nina matumaini makubwa na ninaapa kupaisha gari langu kuhakikisha namaliza katika nafasi tatu za kwanza,” Wahome alieleza Taifa Leo mnamo Septemba 16.

Madereva hao watatu, ambao wanadhaminiwa na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, wameshiriki mashindano kadhaa msimu huu ikiwemo duru ya dunia ya Safari Rally mwezi Juni.

Katika duru ya tano ya KNRC, ambayo ilifanyika katika kaunti ya Machakos, Wahome, 22, alimaliza nafasi ya tano.

McRae Kimathi,26, alikamilisha nje ya mduara wa 10-bora naye Hamza,22, alijiuzulu katika duru hiyo pamoja na ile ya Afrika ya Oryx Energies nchini Tanzania baada ya gari lake kukumbwa na hitalafu ya kimitambo.

Wote watatu watakuwa wakishiriki Ramisi Rally kwa mara ya kwanza kabisa. Kimathi na Wahome wataendesha magari ya Ford Fiesta R3 wakidhaminiwa na Safaricom naye Hamza atatumia gari la Mitsubishi Evolution.

Mradi wa FIA Rally Star unahusisha dunia nzima. Unalenga kutambua, kufundisha na kukuza vipaji vya madereva walio kati ya umri wa miaka 17 na 27. Katika eneo la Afrika Mashariki, Wakenya Hamza Anwar, Mc Rae Kimathi na Jeremy Wahome pekee ndio wako katika mradi huo.

  • Tags

You can share this post!

Kocha wa Ingwe atarajiwa kuwasili Ijumaa

Jambojet yazindua safari za Lamu