• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Real Madrid wazamisha Valencia na kutua kileleni mwa La Liga

Real Madrid wazamisha Valencia na kutua kileleni mwa La Liga

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walifunga mabao mawili katika dakika nne za mwisho wa mchuano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) dhidi ya Valencia na kusajili ushindi wa 2-1 uliowapaisha hadi kileleni mwa jedwali kwa alama 13.

Vinicius Jr alipokezwa krosi na Karim Benzema na kombora lake likababatiza mchezaji wa Valencia kabla ya kujaa ndani ya wavu kunako dakika ya 86.

Dakika mbili baadaye, wanasoka hao wawili walibadilishana majukumu huku Vinicius Jr ambaye ni raia wa Brazil akimpokeza Benzema krosi iliyompa fursa ya kufunga bao lake la sita msimu huu.

Ingawa Valencia walikuwa wamewekwa kifua mbele na Hugo Duro katika dakika ya 66, walishindwa kuhimili presha kutoka kwa wageni wao wanaotiwa makali na kocha Carlo Ancelotti.

Ingawa hivyo, Valencia ndio waliopata nafasi nyingi zaidi za kufunga mabao huku Maxi Gomez na beki Gabriel wakimwajibisha vilivyo kipa Thibaut Courtois.

Katika kipindi cha pili, Goncalo Guedes alipoteza nafasi kadhaa za wazi za kuwaweka Valencia uongozini hadi ushirikiano wake na Duro ulipofaulu. Jaribio la pekee la Real langoni pa Valencia katika kipindi cha kwanza ni kombora la Vinicius Jr ambalo lilidhibitiwa kirahisi na kipa Giorgi Mamardashvili.

Kufikia sasa, Real hawajapoteza mchuano wowote wa La Liga tangu Ancelotti arejee kudhibiti mikoba yao mwishoni mwa msimu wa 2020-21. Miamba hao wameshinda mechi nne na kuambulia sare mara moja katika jumla ya mechi tano za ufunguzi wa muhula huu. Kichapo kutoka kwa Real kilikuwa cha kwanza kwa Valencia kupokea msimu huu.

Huku Real wakiselelea kileleni kwa alama 13, Valencia wanakamata nafasi ya tatu kwa alama 10 sawa na Real Sociedad waliolazimishiwa sare tasa na Sevilla mnamo Jumapili.

Matokeo ya La Liga (Septemba 19, 2021):

Valencia 1-2 Real Madrid

Mallorca 0-0 Villarreal

Real Sociedad 0-0 Sevilla

Real Betis 2-2 Espanyol

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wanasiasa wang’ang’ania mahasla

Haaland abeba Borussia Dortmund dhidi ya Union Berlin ligini