• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
WANGARI: Elimu ya juu iwekeze zaidi katika ujuzi wa kiufundi na kitaaluma

WANGARI: Elimu ya juu iwekeze zaidi katika ujuzi wa kiufundi na kitaaluma

Na MARY WANGARI

WATAHINIWA waliokamilisha mitihani yao ya Cheti cha Elimu ya Sekondari Nchini (KCSE) wataanza kujiunga na taasisi za elimu ya juu wiki hii.

Maelfu ya watahiniwa hao tayari wamepokea barua za mialiko kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali vya umma na vya kibinafsi, huku baadhi wakijiandaa kujiunga na taasisi za kiufundi kote nchini.

Kwa hakika, ni jambo la kufurahia na kuhuzunisha kwa pamoja hasa kwa kuzingatia mamia ya mahafali wanaozidi kutaabika kwa kukosa ajira hata baada ya kufuzu kwa shahada za digrii, uzamili na uzamifu.

Kisa cha hivi majuzi kuhusu Wakenya watatu wenye umri wa makamo kutoka Kaunti ya Homa Bay, waliolazimika kufundisha shule za chekechea licha ya kuwa na vyeti vya uzamifu, ni ithibati tosha ya uhalisia mchungu uliopo.

Viwango vya ajira vingali chini mno nchini licha ya Kenya kuwa miongoni mwa mataifa yanayokua kwa kasi zaidi kiuchumi barani Afrika.

Hali hii imewafanya mahafala wengi waliokuwa na matumaini makubwa kuhusu mustakabali wao kukata tamaa huku baadhi yao wakijitosa katika uhalifu ili kupata riziki.

Kwa kuzingatia hilo, umuhimu wa kuwepo mfumo jumuishi unaotilia maanani ujuzi wa kiufundi na kitaaluma, hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.

Kwa miaka mingi, ukosefu wa wafanyakazi wenye ujuzi umekuwa kero kuu ambayo imegharimu pakubwa mashirika ya umma na ya kibinafsi mamilioni ya fedha huku yakilazimika kusafirisha wataalamu kutoka mataifa ya kigeni nchini.

Ili kuziba pengo hilo, serikali inapaswa kushirikiana na wadau husika kuimarisha taasisi zinazotoa mafunzo na ujuzi wa kitaaluma utakaowezesha vijana kustawi nyanjani.

Taasisi hizo zitawezesha kuwepo kwa watu walio na ujuzi unaohitajika viwandani hivyo kufanya iwe rahisi kwao kupata ajira pindi wanapokamilisha mafunzo yao.

Ili Kenya iweze kufanikisha Ruwaza ya 2030 kuhusu ajira na maendeleo kiuchumi, ni sharti ihakikishe kuwepo kwa wafanyakazi walio na ujuzi unaohitajika katika taaluma husika.

Njia mojawapo ya kufanikisha hayo ni kwa kuwekeza katika taasisi zinazotoa mafunzo ya kiufundi ili kuhakikisha ukuaji na ustawi kiuchumi kwa jumla.

Serikali imejitahidi kuanzisha vituo vya kiufundi kote nchini ikiwemo kuwezesha wanafunzi kupata mikopo na ufadhili wa masomo kujiendeleza kielimu.

Masomo ya vyuo vikuu ni muhimu lakini ni sharti tuende na majira kwa kufanyia mageuzi mfumo wa elimu ya juu nchini.

Kando na kuwezesha vijana kupata ajira, mfumo unauopa kipaumbele ujuzi kiufundi na kitaaluma utaimarisha mustakabali wa Kenya kwa kubuni mikakati jumuishi ya ukuaji na ustawi kiuchumi.

[email protected]

You can share this post!

Dereva amrejeshea mwanafunzi laputopu na Sh20,000...

Covid-19: Majaribio kufanikisha utoaji chanjo kwa watoto wa...