• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Dereva amrejeshea mwanafunzi laputopu na Sh20,000 alizosahau kwenye matatu

Dereva amrejeshea mwanafunzi laputopu na Sh20,000 alizosahau kwenye matatu

Na LAWRENCE ONGARO

DEREVA amemrejeshea mwanafunzi wa chuo kimoja laputopu na Sh20,000 alizosahau kwenye matatu.

Bw Baselio Kimani alipohojiwa alisema nafasi yake haingemruhusu kuchukua kipakatalishi na pesa zilizoachwa ndani ya matatu hiyo.

Matatu hiyo ni ya kuhudumu katika maeneo ya Thika-Kangari-Kandara.

Alisema kwamba mwanafunzi huyo mnamo Jumamosi alikuwa ameabiri matatu ya kutoka Mwea kuelekea Thika huku akishuka kwenye steji ya Blue Post mjini Thika.

Kutoka hapo alipanda matatu ya kutoka Thika kuelekea Kandara ikipitia Kangari.

Lakini kwa ghafla alipofika Kandara alishuka bila mizigo yake.

“Ilinibidi nirudi hadi kituo cha magari ili kujua hasa ni nani pengine alikuwa na mizigo yangu. Bahati nzuri niliona ya kwamba mizigo yangu yote ilirejeshwa,” alijitetea mwanafunzi huyo Ian John Gitau.

Mwanafunzi huyo alitaja tukio hilo kama muujiza kwake kwa sababu “wananchi wengi wana njaa ya pesa.”

Mwanafunzi huyo alisema Mungu ni mkubwa kwa sababu ameonyesha hali ya uvumilivu kwa upande wa dereva huyo.

Dereva alisema tangu utotoni hajakuwa na tamaa kwa kile sio chake.

“Mimi tangu utotoni Mwangi sijakula kitu ya mtu yeyote na wakati mwingi hujishughulisha na mambo yangu mwenyewe.

Bi Lucy Wanjiru ambaye ni mama yake mwanafunzi huyo alisema dereva huyo ni muhimu akapewe tuzo na serikali kwa tukio hilo kwa kuonyesha uzalendo.

kulingana na wale walioshudia tukio hilo, walimtaja dereva huyo kama mtu mwenye uwazi na uwajibikaji.

Jambo hilo limeacha watu wakiendelea kupiga gumzo wakisema kama ingekuwa ni wao hawangetangaza mali hiyo ya mwenyewe bali wangechukua.

Bi Wanjiru aliitaka serikali ifanye juhudi kuona ya kwamba anapokea tuzo zinazopewa watu waliotambulika.

Bi Wanjiru alisema wasafiri na wafanyakazi wa sekta ya uchukuzi popote walipo waendelee kuiga mfano wa Bw Kimani ambaye alionyesha umaarufu wake kwa kujali maslahi ya mwanafunzi huyo.

You can share this post!

Mfahamu Jarred Gillett ambaye sasa atakuwa refa wa kwanza...

WANGARI: Elimu ya juu iwekeze zaidi katika ujuzi wa...