Na MASHIRIKA
ACCRA, GHANA
GHANA imesema itayapiga mashirika ya ndege faini ya Sh350,000 kwa kila abiria anayeingia nchini humo bila cheti cha chanjo ya Covid-19.
Chini ya masharti hayo ambayo yanaanza kutekelezwa leo Jumatano, mashirika hayo pia yatapigwa faini ikiwa abiria hawatakuwa wamejaza fomu maalum ambayo imetolewa na wizara ya afya nchini humo.
Ijapokuwa raia wa taifa hilo ambao wataingia humo bila kutimiza kanuni hizo watawekwa karantini kwa siki 14, raia wa kigeni watakuwa hatarini kuzuiwa kuingia nchini humo.
Ghana ni miongoni mwa nchi ambazo zimeanza kuchukua tahadhari kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, baada ya virusi aina ya Omicron kugunduliwa nchini Afrika Kusini mnamo Novemba.