• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 5:23 PM
Ada ya juu ya umeme yanyima raia maji safi

Ada ya juu ya umeme yanyima raia maji safi

Na SIAGO CECE

ULIMWENGU uliadhimisha Siku ya Maji Ulimwenguni Jumatatu huku ada ya juu ya stima ikitajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa wakazi wa Mombasa kupata huduma ya maji safi.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabomba na Usambazaji Maji ya Mombasa (Mowasco), Bw Anthony Njaramba, alisema wakazi wengi wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji.

Akizungumza na Taifa Leo wakati wa kuadhimisha siku ya maji ulimwenguni, Bw Njaramba alisema bili hizo za juu za kampuni ya Kenya Power zimesababisha Mowasco kuwapunguzia wakazi kiwango cha maji wanayopokea.

“Tatizo kuu ni ada ya juu ya stima. Ikiwa ada yenyewe ingekuwa chini, maji zaidi yangesukumwa kwenye nyumba za watu. Kutokana na hali hii, idadi ya wakazi wa Kaunti ya Mombasa wanaopokea maji kwenye mifereji yao ni ndogo mno,” alieleza.

Kwa sasa ni asilimia 15, (chini ya laki moja) ya zaidi ya wakazi milioni moja katika kaunti hiyo wanaopata maji. Kaunti ya Mombasa, kutokana na kuwa sehemu kubwa ipo kando ya bahari, maji yake huwa na ladha ya chumvi. Kwa hivyo wakazi hutegemea maji yanayosambazwa na Mowasco kwa matumizi ya nyumbani.

Ili kutatua shida hiyo ya uhaba wa maji, Bw Njaramba alisema wanalazimika kuwapimia maji wakazi.

“Tunapima maji kulingana na maeneo. Tunafungua kwa siku maalumu. Hii ni kuwezesha kila mtu apate maji, hata kama ni kiwango kidogo,” akasema.

Katika kaunti ndogo ya Mvita, wakazi hupata maji siku nne pekee kwa wiki. Maeneo ya Changamwe hupata maji safi mara moja kwa wiki.

Alieleza kuwa hata wafanyibiashara walio na viwanda vya kusafisha maji ya chumvi, wanakumbwa na changamoto hiyo ya ada ya juu stima.

Bw Njaramba pia alisema visa vya wizi wa maji, hasa kwa maeneo ambayo yanakosa maji, vimeongezeka.

“Kila eneo la Mombasa lina wezi wa maji. Hatuwezi kusema kuwa kuna eneo moja ambalo lina wezi zaidi. Wengi wanaiba maji hayo na kuyauza kwa bei ya juu,” alieleza.

Ili kukabiliana na haya, wakazi wengi wamechimba visima nyumbani kwao. Wengine pia wanatumia mashine maalum ya kutengeza maji safi.

Kila mwezi, mitaa ya Mombasa hasa Changamwe huwa yanakosa maji safi ya kunywa huku wakazi wakitegemea wafadhili wanaogawa maji ya bure.

Maeneo mengine yanayokosa maji ni Bamburi, Kisauni, Likoni na Bombolulu.

Hata hivyo, serikali ya kaunti ya Mombasa imesimamisha mipango ya kutengeza kiwanda cha kusafisha maji kwa muda kwa sababu ya virusi vya corona.

Waziri wa Maji, Bi Mariam Mbaruk alisema kiwanda hicho kilifaa kutatua changamoto ya maji safi Mombasa lakini bado mazungumzo baina yao na serikali kuu yanaendelea kabla ya mradi huo kuanza.

 

  • Tags

You can share this post!

Rais apigiwa makofi kwa kukatiza hotuba juu ya maombi

Manchester City sasa wanamtaka mfumaji Danny Ings wa...