• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Manchester City sasa wanamtaka mfumaji Danny Ings wa Southampton awe kizibo cha Aguero ugani Etihad

Manchester City sasa wanamtaka mfumaji Danny Ings wa Southampton awe kizibo cha Aguero ugani Etihad

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City wanahemea huduma za fowadi Danny Ings wa Southampton ili awe kizibo cha mshambuliaji matata raia wa Argentina, Sergio Aguero.

Mustakabali wa Aguero uwanjani Etihad bado haujulikani huku akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua Barcelona baada ya mkataba wake na Man-City kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu.

Japo kocha Pep Guardiola amefichua kwamba azma yake ilikuwa ni kumtwaa Erling Haaland wa Borussia Dortmund ili kujaza nafasi ya Aguero, kima cha Sh14 bilioni kinachodaiwa na waajiri wa sasa wa Haaland ni cha juu sana.

Kujiondoa kwa Man-City katika mbio za kufukuzia saini ya Haaland sasa kunawaweka Real Madrid, Manchester United na Chelsea katika nafasi nzuri zaidi ya kujinyakulia huduma za fowadi huyo chipukizi raia wa Norway.

Ings, 28, amefufua pakubwa makali yake katika soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) tangu abanduke kambini mwa Liverpool na kuingia katika sajili rasmi ya Southampton mnamo 2019.

Ushawishi wake uwanjani, hasa katika safu ya mbele, ni kiini cha kocha Gareth Southgate kumrejesha katika kikosi cha Uingereza kinachojiandaa kwa mechi tatu zijazo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Ings alipachika wavuni jumla ya mabao 22 katika kampeni za EPL mnamo 2019-20 na akawa miongoni mwa wafungaji bora wa kipute hicho.

Kikubwa zaidi kinachowapa Man-City msukumo wa kutaka kumsajili ni unafuu wa bei ambayo watafanikiwa kumpata fowadi huyo nayo ikizingatiwa kwamba kandarasi yake ya sasa na Southampton inatamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2021-22.

Mbali na kuwania maarifa ya Ings, Man-City wanafuatilia pia hali ya kiungo Denis Zakaria kambini mwa Borussia Monchengladbach nchini Ujerumani kwa matumaini kwamba watamsajili muhula huu katika jaribio la pili la kumtwaa.

Man-City ambao kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 71, pia wanafukuzia jumla ya mataji matatu mengine yakiwemo Kombe la FA, Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na League Cup.

Kitavaana na Chelsea kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA kabla ya kuchuana na Tottenham Hotspur kwenye fainali ya League Cup mnamo Aprili 25, 2021.

Iwapo Man-City watawacharaza Dortmund kwenye robo-fainali ijayo ya UEFA, basi watajikatia tiketi ya nusu-fainali ambapo watakutana ama na Bayern Munich ya Ujerumani au Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ada ya juu ya umeme yanyima raia maji safi

Vita vya serikali na usimamizi wa KTDA