• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Afueni ya wamiliki wa baa Mlima Kenya washukiwa wa wizi wa pombe wakitiwa mbaroni

Afueni ya wamiliki wa baa Mlima Kenya washukiwa wa wizi wa pombe wakitiwa mbaroni

NA LABAAN SHABAAN

WAMILIKI wa baa katika Kaunti za Meru, Tharaka Nithi, Embu, Laikipia na Kirinyaga wana sababu ya kutabasamu baada ya washukiwa wa wizi ambao huvunja biashara zao na kuiba pombe kukamatwa na polisi.

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imetangaza kutiwa mbaroni kwa washukiwa kumi na kutwaa kreti za pombe na vifaa vingine.

“Bonface Mutwiri, Patrick Mwenda, David Mwaki, Gideon Gatobu, Sharon Makena, Fidelis Kananu, Abdullahi Yusuf, Caroline Kanana, Bonface Kathiri na Martin Mwiti walikamatwa katika operesheni kali ya makachero,” ilithibitisha DCI kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X.

Uchunguzi na msako katika kituo cha burudani cha Stinger Lounge Bar unaendelea ili kumnasa mmiliki wake Geoffrey Muriuki anayeaminiwa kupanga njama za wizi wa kimabavu.

Ndani ya baa hili, mlipatikana vitu vilivyoibwa vikijumuisha pombe, pampu na mitungi ya kileo cha keg.

DCI inasema washukiwa hawa walikamatwa eneo la Makutano wakiwa na magari matatu yenye panga na vyuma vinavyoaminika kutumika kuvunja vilabu.

Kadhalika, uchunguzi wa wapelelezi uliwawezesha kupata nambari kadhaa za usajili wa magari, simu, runinga na kamera zinazodhaniwa kuwa za wizi.

Polisi wanaendeleza msako wa mshukiwa mkuu Geoffrey Muriuki ambaye yuko mafichoni huku wenzake wakitarajiwa kufikishwa mahakamani Jumanne asubuhi.

  • Tags

You can share this post!

Malala halali: UDA wafungua ofisi mpya Kisumu kunasa...

Mali ya Bunge la Kaunti ya Machakos hatarini kupigwa mnada...

T L