• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Malala halali: UDA wafungua ofisi mpya Kisumu kunasa wafuasi 200,000

Malala halali: UDA wafungua ofisi mpya Kisumu kunasa wafuasi 200,000

NA LABAAN SHABAAN

CHAMA tawala cha United Democratic Alliance kimefungua ofisi mpya Kisumu Magharibi ili kunasa wafuasi katika ngome ya kisiasa ya Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga.

Ufunguzi huu unajiri miezi michache baada ya ofisi nyingine ya UDA kuteketezwa eneo la Milimani, Kisumu wakati wa maandamano dhidi ya serikali.

Akizindua ofisi hiyo, Mwenyekiti wa UDA Kaunti ya Kisumu James Odhiambo Oyolo alisema ufunguzi wa kituo cha eneobunge unalenga kufanya chama hicho maarufu eneo la Nyanza.

“Tunataka chama kienee Nyanza kwa sababu Raila Odinga alileta mfumo wa vyama vingi. Sisi tulikuwa wana-ODM, sasa tumehamia UDA na tunataka kutafuta wanachama wa UDA ili ukifika mwaka wa 2027 wampigie kura Rais William Samoei Ruto,” Bw Odhiambo alisema alipokata utepe kufungua kituo hicho.

Maafisa wa chama tawala wanasema kuwa wanalenga kuvuna wafuasi 200, 000 katika mpango mpya wa kusajili wanachama unaoendelea.

Huku usajili ukiendelea kote nchini, Rais William Ruto ametaka vyama vyote vilivyo chini ya mwavuli wa Kenya Kwanza kufunga vyama vyao na kujiunga na UDA.

Rais alisema haya alipohutubu katika mkutano wa Baraza la Kitaifa la Usimamizi wa Chama (NGC) mnamo Septemba 29, 2023 ukumbini Bomas of Kenya jijini Nairobi.

Akiamini kuwa na chama kimoja kutasaidia kutekeleza manifesto ya serikali, kiongozi wa taifa alisema hakuna chama kinafaa kulazimishwa kujiunga na UDA.

Ofisi ya UDA Kisumu Magharibi iliyozinduliwa na Mwenyekiti wa UDA Kaunti ya Kisumu James Odhiambo. PICHA | NATION
  • Tags

You can share this post!

Utafiti wakanusha; ‘stress’ haisababishi...

Afueni ya wamiliki wa baa Mlima Kenya washukiwa wa wizi wa...

T L