• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Aina hatari ya corona imetua nchini – Kagwe

Aina hatari ya corona imetua nchini – Kagwe

Na BENSON MATHEKA

Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, amekiri kwamba visa vya maambukizi ya aina mpya hatari ya corona iliyogunduliwa Afrika Kusini na Uingereza vimethibitishwa nchini.

Hata hivyo, Bw Kagwe aliondolea Wakenya hofu kuhusu athari za aina hizo akisema inayoambukiza watu wengi nchini ni ile iliyothibitishwa Kenya mwaka jana.

“Aina ya virusi vya corona inayosambaa Kenya kwa wingi ni iliyothibitishwa nchini mwaka jana. Hata hivyo, kumekuwa na visa vya aina mpya iliyogunduliwa Afrika Kusini na Uingereza,” Bw Kagwe alisema jana.

Kenya inakumbwa na wimbi la tatu la maambukizi ya corona ambayo yamefanya serikali kuchukua hatua za kuikabili kwa kufunga kaunti tano za Nairobi, Machakos, Kiambu, Kajiado na Nakuru. Akitangaza kufungwa kwa kaunti hizo mnamo Ijumaa wiki jana, Rais Uhuru Kenyatta alisema zimechangia asilimia 70 ya maambukizi ya virusi hivyo nchini.

Idadi ya maambukizi na vifo vinavyosababishwa na virusi hivyo inaendelea kuongezeka huku nchi ikikumbwa na uhaba wa oksijeni.

Bw Kagwe alisema kuna viwanda 75 vya oksijeni nchini ingawa baadhi havifanyi kazi.

Waziri Kagwe alisema oksijeni ni silaha muhimu katika vita dhidi ya janga la corona wagonjwa wanapolazwa hospitalini. Mnamo Ijumaa, Rais Kenyatta alisema zaidi ya Wakenya 950 walikuwa wamelazwa na katika vyumba vya wagonjwa mahututi na maelfu walikuwa wameongezewa oksijeni kuwasaidia kupumua. Aliagiza serikali za kaunti kushirikiana na Wizara ya Afya kuthibitisha kiwango cha oksijeni nchini. Rais Kenyatta aliagiza oksijeni iliyoko nchini itengwe kwa vita dhidi ya corona pekee.

Jana, Bw Kagwe alisema kiwango cha oksijeni nchini kinatishiwa na mambo kadhaa vikiwemo viwanda visivyofanya kazi.

Alisema moja ya changamoto kuu ni kuwa, mitungi 20,000 ya oksijeni iko katika nyumba za watu na taasis mbalimbali.

“Wanatakiwa kuirudisha mara moja, ni makosa kuweka mitungi hiyo huku watu wakifariki kwa kukosa oksijieni,” alisema.

You can share this post!

Sossion aililia serikali shule zifunguliwe Mei

Mshtuko huku corona ikiua maafisa 5 wa kaunti