• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Aina hatari zaidi ya corona yagunduliwa TZ

Aina hatari zaidi ya corona yagunduliwa TZ

Na BENSON MATHEKA

AINA hatari zaidi ya virusi vya corona imekuwa ikisambaa Tanzania, inasema ripoti iliyowasilishwa kwa Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, na mtaalamu wa afya.

Ripoti hiyo inasema kwamba, aina hiyo imebadilika mara kadhaa kuliko aina nyingine zilizotambuliwa kufikia sasa kote ulimwenguni.

Ripoti hii inajiri siku moja baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo John Magufuli ambaye alilaumiwa kwa kupuuza kanuni za kuzuia corona kuzikwa Ijumaa.

Kulingana na mwanasayansi Tulio de Oliveira, mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa matibabu za Krisp, wataalamu wake walipata aina hiyo mpya imeambukiza wasafiri waliotoka Angola na Tanzania.

Kituo hicho kilisema kwamba, kitaendelea kuchunguza aina hiyo mpya ya corona kubaini inavyoathiri kinga ya mwili.

Hakuna mengi yanayojulikana kuhusu hali ya corona Tanzania ambayo chini ya Magufuli iliacha kutoa habari kuhusu virusi hivyo mapema 2020.

Magufuli alizikwa Ijumaa, siku tisa baada ya maafisa wa serikali kutangaza kwamba alifariki kutokana na matatizo ya moyo.

Maafisa kadhaa wa serikali yake waliuawa na virusi hivyo lakini akaendelea kuhimiza raia kutotishika akikejeli nchi zilizochukua hatua za kuzuia msambao wa virusi hivyo.

Maafisa wa WHO wanahofia kuwa, huenda kiwango cha maambukizi nchini humo kiko juu. Mnamo Ijumaa, Rais Samia Suluhu alitangaza kuwa atafuata nyayo za mtangulizi wake Magufuli.

Tanzania imekataa chanjo ya kuzuia corona ambayo imekumbatiwa na mataifa mengine ulimwenguni.

Aina tofauti za virusi hivyo barani Afrika viliripotiwa Afrika Kusini na Nigeria.

You can share this post!

Thierry Henry ajiondoa kwenye mitandao ya kijamii...

Watahiniwa watasaidiwa kusafiri – Oguna